Urusi imetoa chanjo ya kwanza ya kulinda wanyama kutokana na virusi vya corona (Covid-19).
Shirika la ukaguzi wa bidhaa za kilimo na mifugo la Urusi Rosselhoznadzor, liliripoti kwamba toleo la kwanza la chanjo inayoitwa Carnivac-Cov, ambayo italinda wanyama dhidi ya virusi vya corona aina ya Sars-Cov-2 vinavyosababisha na ugonjwa wa Covid-19, ilitolewa kwa kiwango cha dozi elfu 17.
Mshauri wa Rosselkhoznadzor, Yuliya Melano, alisema kuwa kwa sasa wana uwezo wa kutoa dozi milioni 3 za chanjo kwa mwezi, na kwamba hii inaweza kuongezeka hadi dozi milioni 5 kwa kuzingatia mahitaji.
Melano pia alisema kuwa kampuni za Ujerumani, Ugiriki, Poland, Austria, Kazakhstan, Tajikistan, Malaysia, Thailand, Korea Kusini, Lebanon, Iran na Argentina zinataka kununua chanjo hiyo.
Mshauri wa Rosselkhoznadzor aliongezea kusema,
"Karibu mashirika 20 yalisema kuwa yapo tayari kujadili idhini ya chanjo ya Carnivac-Cov na usambazaji wake kwa nchi zao. Stakabadhi inayohitajika kwa idhini ya chanjo hiyo nje ya nchi, haswa katika Jumuiya ya Ulaya, inaandaliwa na itatumika katika mchakato wa idhini ya chanjo hiyo."
Chanjo inayoitwa Carnivac-Cov ilisajiliwa nchini Urusi mnamo Machi baada ya kubainika kuwa ilitoa kingamwili dhidi ya virusi vya corona kwa mbwa, paka, mbweha na pimbi wakati wa majaribio yake.
Maafisa wa Shirika la Afya Ulimwenguni hapo awali walisema kwamba wana wasiwasi juu ya maambukizi ya corona kati ya wanadamu na wanyama.
Maafisa wa Rosselkhoznadzor wanasema kuwa wanaamini chanjo ya Carnivac-Cov inaweza kulinda spishi za wanyama walio hatarini na kuzuia mabadiliko ya virusi.