JIJI la Arusha juzi lilikuwa na hekaheka kubwa ya kushuhudia ndoa ya mtoto wa Nabii wa Nigeria, Temitope Balogun Joshua maarufu kama TB Joshua, Serah Joshua iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Moyo safi wa Bikira Maria iliyopo Unga Limited.
Ndoa hiyo ya Serah Joshua kwa Mtanzania Brian Moshi ilifungwa na Paroko wa Kanisa hilo, Festus Mangwangi. Binti huyo ni miongoni mwa watoto watatu wa T B. Joshua aliyezaliwa Juni 12, 1963.
TB Joshua ni mmoja ya manabii maarufu na mwasisi wa Kanisa la The Synagogue, Church of All Nations (SCOAN), kanisa linaloendesha pia televisheni ya Emmanuel yenye matangazo ya kikristo kutoka Lagos , Nigeria.
Akihubiri wakati wa kufungisha ndoa hiyo, Paroko Mangwaji alisema kufungwa kwa ndoa hiyo kumeiunganisha nchi ya Tanzania na Nigeria.
Alisema ndoa hiyo ni ushuhuda wa malengo ya Hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere ya kutaka Bara la Afrika liwe kitu kimoja na kuwa sasa yametimia baada ya ndoa hiyo.
Padre Mangwaji alisema yapo mengi yanayounganisha watu ikiwa ni pamoja na masomo na kuoana na kuwa yanapotokea mambo hayo huondoa uwezekano wa kubaguana.
“Serah huko Nigeria umeona wanaume wengi lakini umempenda Brian na Brian hapa Sinoni au Marekani uliona wengi lakini umemchagua Serah, wanangu nawaombea mkazae matunda mema kwa sifa na Utukufu wa Mungu,” alisema.
Alisema ndoa hiyo ya mume na mke mmoja kwa taratibu za Kanisa Katoliki, ilitangazwa kanisani hapo mara tatu kuanzia Aprili 11,2021 hadi Mei 2,2021 na hakukuwa na pingamizi lolote na kuamua ifungwe.
Padre Mangwaji aliwataka maharusi hao kuzaa watoto nane ili Kanisa lipate watawa na kuja kuwasaidia katika kazi ya kuhuburi neno la Mungu. Ndoa hiyo ilihudhuriwa na wageni kutoka Lagos, Nigeria na Marekani, wanaposoma Brian na Serah.
Mke wa Tb Joshua na mama wa Serah, Evelyn Joshua alisema hii ni mara ya kwanza kuja nchini Tanzania na amekuja kushuhudia ndoa ya mtoto wake.
Alitumia pia alitumia nafasi ya harusi hiyo kushukuru muungano huo na kuongeza kuwa anacho cha kusimulia akirudi nchini Nigeria.
Desemba, 2020, Nabii TB Joshua alishindwa kuhudhuria harusi ya binti yake nchini humo kutokana na maagizo yanayolingana na waji bu wake.
Kwa mujibu wa mtandao wa Opera News TB Joshua alikuwa anapokea maagizo kwa ajili ya mwaka 2021. Aidha alisema kwamba kuna umuhimu wa kusikiliza maneno ya Mungu hata ni magumu sana kwako.