LICHA ya timu ya Manchester United kupewa asilimia kubwa ya kushinda taji la Europa League mambo yamekuwa magumu kwao baada ya kuliacha mikononi mwa wapinzani wao ambao walikuwa hawapewi nafasi.
Villarreal inayonolewa na Unai Emery imeibuka na ubingwa huo mbele ya Manchester United katika mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia leo kwa ushindi wa penalti 11-10 baada ya sare ya kufungana bao 1-1.
Gerrard Moreno alianza kupachika bao kwa Villarreal likawekwa usawa na Edinson Cavani.
Ilikuwa ni bonge moja ya fainali kwa kuwa dakika 30 ziliongezwa na ngoma ikawa sare ya 1-1, jumla ya penalti 22 zilipigwa na 21 zote zilizama nyavuni, ilikuwa penalti ya kipa namba moja wa United, David de Gea iliamua ubingwa uende kwa Villarreal kwa kuwa kipa alidaka.
United Mara ya mwisho kutwaa taji hilo ilikuwa 2017 zama za Kocha Mkuu, Jose Mourinho hivyo bado anaendelea kushikilia rekodi yake.
Unai anaweka rekodi yake ya kuingia fainali mara ya kwanza na timu hiyo na kusepa na taji jumlajumla jambo linalomfanya awe na bahati na taji hilo kwa kuwa aliwahi kutwaa taji hilo zama alipokuwa akifundisha pia Sevilla.