Vinara wa Wizi Wanaswa Mbeya





KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA MATUKIO YA UVUNJAJI NA WIZIy

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili 1. KELVIN TOBIAS [32] fundi kuchomelea, mkazi wa Iyela na 2. JOSHUA AMBAKISYE [18] mkazi wa Mwanjelwa jijini Mbeya kwa tuhuma za kujihusisha na matukio mbalimbali ya uvunjaji na wizi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya.

Watuhumiwa wamekamatwa katika misako inayoendelea katika maeneo mbalimbali ndani ya Jiji la Mbeya na wamekiri kujihusisha na matukio ya uvunjaji na wizi. Katika upekuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya katika maeneo ambayo watuhumiwa wamekiri kuuza mali za wizi, mali zifuatazo zimepatikana:-

 

    Kompyuta 2 [Desk top] aina ya HP,
    Laptop 2 aina ya HP na Dell.
    CPU 2 aina ya Dell,
    TV flat screen aina ya Hicence inchi 55,
    TV flat screen aina ya LG inchi 32,
    TV flat screen aina ya Singsung inchi 32,
    TV flat screen aina ya Samsung inchi 32,
    Mitungi miwili mikubwa ya gesi Oryx,
    Mitungi mitatu midogo ya gesi Oryx,
    Redio Sub-woofer 6 aina tofauti,
    Jiko moja la Gesi aina ya Afrox,
    Blanketi 13,
    Saa 2 za ukutani na
    Redio 2 mali ya wizi.
 

Upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa matukio ya uvunjaji na wizi wa mali mbalimbali. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi walioibiwa mali zao kufika kituo kikuu cha Polisi Mbeya Mjini kwa ajili ya  utambuzi wa mali zao.

KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA TUKIO LA MAUAJI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa GODLOVE PIMBI [50] Mkazi wa Lusonjo – Kisyosyo kwa tuhuma za mauaji ya mke wake aitwaye ELIZABETH MWAIKE [22] Mkazi wa Lusonjo – Kisyosyo.

Tukio hili limetokea mnamo tarehe 11.05.2021 nyumbani kwa mtuhumiwa huko Kijiji cha Kisyosyo kilichopo Kata ya Matema, Tarafa ya Ntebela, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya.

Chanzo cha tukio hili ni wivu wa kimapenzi. Mwili wa marehemu ulikutwa umbali wa mita 500 kutoka nyumbani kwake ukiwa na jeraha la kupigwa na kitu kizito kichwani. Upelelezi wa tukio hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa rai kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya migogoro ya kimapenzi na badala yake watafute suluhisho kwa kukaa meza moja ya mazungumzo ili kutatua migogoro hiyo.

ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA MAUAJI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia CHIKU ABOUBAKARI [41] Mkazi wa DDC – Mbalizi kwa tuhuma za mauaji ya ROSE MWANDANJE [45] Mfanyabiashara na Mkazi wa DDC – Mbalizi.

Tukio hilo limetokea tarehe 11.05.2021 majira ya saa 20:00 usiku huko Mtaa wa DDC – Mbalizi uliopo Kata ya Utengule – Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya ambapo marehemu ROSE MWANDANJE [45] Mkazi wa DDC – Mbalizi aliuawa kwa kukatwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo nyuma ya shingo na viganja vya mikono yote kutoka na mtu / watu wasiofahamika akiwa sebuleni katika nyumba anapoishi.

Chanzo cha tukio hilo kinachunguzwa. Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea na msako mkali dhidi ya watuhumiwa wengine waliohusika katika tukio hilo la kinyama. Aidha Jeshi la Polisi linaendelea kutoa rai kwa wananchi na watendaji wa mitaa kutoa ushirikiano kwa kuwafichua wahalifu ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.


MTU MMOJA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUANGUKIWA NA KIFUSI.

Mtu mmoja aitwaye MWASHALA NYUNDURU [32] Mkazi wa Kabwe Jijini Mbeya alifariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi cha mchanga akiwa anafanya shughuli za uchimbaji mchanga katika eneo la Shewa.

Tukio hili limetokea tarehe 11.05.2021 majira ya saa 17:33 jioni huko maeneo ya Mtaa wa Shewa, Kata ya Mwakibete, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya wakati marehemu akiendelea na shughuli za uchimbaji mchanga akiwa na wenzake. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wakiwa katika shughuli za uchimbaji ili kuepuka madhara yanayoweza kuepukika hasa katika kipindi hiki ambacho mvua za mwishoni zinaendelea kunyesha.

 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad