Wanawake msiwadharau wanaume, ukiwa na fedha saidiana na mumeo - DC Asia Abdallah






Wanawake mkoani Iringa wamekumbushwa kuacha tabia ya kuwadharau wanaume wanapokuwa na kipato ili kulinda ndoa zao.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili 4, 2021 na mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah wakati akifungua warsha ya fursa kwa  wanawake katika misitu  wilayani Mufindi.

Amesema wanawake watumie fursa za kiuchumi wanazozipata huku akiwakumbusha kuheshimu wanaume zao ili kulinda ndoa na watoto.

Amebainisha kuwa mwanamke kujishughulisha na kupata kipato chake ni kwa ajili ya kusaidiana na mumewe kuhudumia familia si kumdharau mwanaume ambaye naye anaweza kufanya kazi na kupata kipato.

“Unapopata fursa ya kupata kipato isiwe ndio chanzo cha  kufanya ndoa kuteteleka..., unafanya biashara  lakini kumbuka unalo jukumu gumu la kuangalia familia na hutakiwi kutenganisha maisha ya familia na biashara yako.”

“Baadhi yetu kusijisahau tukaanza kuwapanda waume zetu vichwani, wanawake wengine wakishaanza kupata fedha wanajisahau,” amesema.

Amewataka wanawake kutumia fursa ya misitu kujipatia kipato kwa kujishughulisha kama ufugaji nyuki, kulima miti na kufanya biashara ya miche.

“Mwanamke ukitoka katika shughuli zako ukifika nyumbani wewe ni mama wa familia ongea na watoto wako washauri katika masuala ya mimba za utotoni na janga la Ukimwi hili sio jukumu la dada wa kazi ni kwa faida ya maisha ya watoto wako,” amesema.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad