Waziri wa Uwekezaji Mhe.Geofrey Mwambe ametoa siku 14 kwa wawekezaji nchini ambao shughuli zao za uwekezaji zimesimama au zimekwamishwa kwa namna yoyote kutokana na maamuzi ya taasisi za Serikali kuandika barua na kuzipeleka wizarani ili kuweza kushughulikiwa.
Ameyasema hayo leo Jijini dar es salaam alipokuwa akizungumza na wafanyakazi pamoja na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Ameongeza kuwa, sekta binafsi zinaweza kuwa na madhaifu mengi hivyo wizara yake iko tayari kukaa na kuziangalia changamoto zinazowakumba wawekezaji na wale wanaotaka kuwekeza nchini ili kujadiliana na kuona namna ya kuwasaidia hali itakayopelekea kuondoa vikwazo kwa wawekezaji na kuweza kuwapa nafasi ya kuwekeza ndani ya nchi.
“Kuna wawekezaji ambao wamekuja na kuanguka hawakufanikiwa kuweza kupata idhini ya kuwekeza hivyo hawa wawekezaji wote waje waandike barua kwetu tutakaa ndani ya wizara tutajadiliana na kuona ni namna gani ya kuwasaidia kutoka pale walipokwama kwenda mbele”, amesema Mwambe.
Aidha Mhe. Mwambe amewataka wafanyakazi wa kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC ) kufanya kazi kwa weredi, kujituma na kwa ushirikiano na kujikita zaidi katika kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya uwekezaji ili kuhakikisha sekta ya uwekezaji inakuwa kwa kiwango kikubwa nchini huku wakijiepusha na vitendo vya rushwa kwani ni kinyume na sheria na taratibu za utumishi wa umma.
“Watumishi tujitahidi kuhakikisha TIC inakuwa juu kwa kutumia weledi mwingi na uzalendo kwani tukilisaidia taifa tutakuwa Wazalendo wa kweli na kutokuchukua rushwa kabisa, rushwa TIC ni marufuku, tunatakiwa tuhakikishe TIC sio sehemu ya rushwa,” amesema Mwambe.
Pamoja na hayo Mhe.Mwambe ameziomba taasisi za Serikali kushirikiana kuyajenga makampuni ya kitanzania yaliyosajiliwa na kufanya kazi hapa nchini ili kuwasababishia wapate faida na serikali ipate fedha nyingi na kuwaonya baadhi ya wafanyabiashara kuwatumia maafisa wa serikali kukandamiza wawekazaji wanaokuja kuwekeza Tanzania vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.