Dar es Salaam. Kampuni ya mtandao wa simu ya Airtel Africa PLC imekubali kuuza minara ya mawasiliano ya Airtel Tanzania inayomilikiwa kwa ubia na kampuni mbili tofauti – SBA Communications Corp na Paradigm Infrastructure Ltd kwa $175 milioni (sawa na Sh400 bilioni).
Airtel imeeleza hayo jana Jumatano Juni 2, 2021 kupitia taarifa yake.
Wakati SBA ni mmiliki na mwendeshaji wa miundombinu ya teknolojia ya mawasiliano isiyohusisha nyaya (wireless communication), Paradigm, kampuni ya Uingereza unalenga kukuza, kumiliki na kuendesha miundombinu ya mawasiliao isiyo na nyaya katika baadhi ya masoko yanayokua.
Mauziano hayo yanatoa mwanya kwa kampuni hiyo kujikita katika biashara yake ya msingi ya kuanzisha na kuendeleza mawasiliano baina ya wateja wake.
Hii ina maana kwamba, minara ambayo awali ilimilikiwa na Airtel, sasa itamilikiwa na kuendeshwa na kampuni tofauti, na kwamba Airtel sasa itakuwa inailipia kulingana na mkataba.
Airtel Tanzania inamiliki minara 1,400, ambayo ni sehemu ya mtandao wa mawasiliano yasiyohusisha nyanya unaoendeshwa na kampuni hiyo.
Airtel's Africa inamiliki kampuni za simu katika nchi 14 ikiwemo Kenya, Uganda, Nigeria Zambia na nchi zingine kadha.