Aisee! Mastaa hawa 10 walishikwa mkono wakajibeba kabisa...



Imekuwa ni kawaida katika siasa, biashara, michezo, muziki, filamu na mitindo, kila anayefanya vizuri upande huo, kuna mtu alimshika mkono au kumvutia kufanya mojawapo kati ya hayo machache.


Je, kwenye muziki wa Bongofleva hali ipoje? Wasanii wamekuwa wakishirikishwa kwenye nyimbo kila siku, lakini kuna wale ambao kufanya hivyo kulipelekea kuleta au kutengeneza majina mapya na baadaye kuwa makubwa kwenye muziki huo. Karibu.


1. Ben Pol > Darassa

Hakuna ubishi kuwa wimbo ‘Sikati Tamaa’ ambao Darassa alimshirikisha Ben Pol ndio uliomtoa mwenyewe kimuziki, licha ya huko nyuma kurekodi nyimbo kibao.


Baada ya miaka zaidi ya mitano Darassa alimshirikisha tena mkali huyu wa RnB katika wimbo uitwao ‘Muziki’ ambao ulipelekea jina la Darassa kuwa kubwa maradufu.


2. Alikiba > Ommy Dimpoz

Wawili hawa walikutana G Records na Prodyuza KTG akawatengenezea mdundo wa wimbo ‘Nai Nai’ ambao Ommy Dimpoz alimshirikisha Alikiba, baada ya hapo jina la Ommy likawa maarufu kila kona.


Na baada ya miaka mingi walitoa wimbo mwingine uitwao ‘Kajiandaye’, huku Alikiba akija kumsainisha Ommy Dimpoz ndani ya Rockstar Africa wakati akiwa kiongozi katika lebo hiyo.


3. Belle 9 > Young Killer

Ngoma yake iitwayo ‘Dear Gambe’ aliyomshirikisha Belle 9 ndiyo ilimtoa na kumpa tuzo ya Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) mwaka 2013 kipengele cha msanii bora chipukizi kwa wakati huo.


Kabla ya wimbo huo, Young Killer ambaye alikuwa akisifika kwa uwezo wa kuandika mistari kwenzi na kuichana, tayari alikuwa amesharekodi baadhi ya nyimbo na Maprodyuza kama D Classic na Duke Tachez.


4. Mwana FA > Maua Sama

Mwimbaji Maua Sama mwenye sauti ya kipekee alikuwa amesharekodi wimbo wake ‘So Crazy’ na Prodyuza mwingine huko Moshi, lakini hakufanya vizuri.


Alipokuja kukutana na Mwana FA wakaifanya upya ngoma hiyo chini ya Prodyuza Marco Chali, na ndio ikawa tiketi ya Maua Sama kusikika kwenye Bongofleva hadi sasa.


5. Belle 9 > Shetta

Wimbo ‘Nimechokwa’ ndio uliomtoa Shetta kimuziki, ni wazi sauti ya Belle 9 kama msanii mkubwa kwa wakati huo ilipelekea wengi kuipenda ngoma hiyo. Kutokana na mafanikio yake, haikuwa ajabu Shetta kuendelea kufanya kolabo na wakali wa kuimba kama Dully Sykes, Tundaman, Diamond Platnumz, Rich Mavoko, Jux n.k na kuzifanya nyimbo zake kuwa kubwa.


6. Jux >Mabeste

Rapa huyu mwenye swaga za muziki wa Genge kutoka Kenya, alitambua sauti ya Jux inafaa katika wimbo wake ‘Baadaye Sana’ ambao ulipokelewa kwa mikono miwili kwenye Bongofleva.


Kolabo hiyo ilirekodiwa na marehemu Prodyuza Pancho chini ya B’Hits Music Group ambapo kwa wakati huo Jux na wenzake kutoka kundi la Wakacha nyimbo zao nyingi walirekodia hapo.


7. Rich Mavoko > Stamina

Rapa huyu anayetamba na kundi Rostam kwa sasa, alimshirikisha Rich Mavoko katika wimbo wake uitwao ‘Kabwela’ na ndipo akatoka kimuziki ingawa alikuwa ameurekodi awali zaidi ya mara tatu.


Kufanya vizuri kwa wimbo huo kulipelekea Stamina kuona umuhimu wa kuchanganya Hip Hop na RnB, ndipo akamshirikisha Jux katika wimbo ‘Alisema’ ambao nao ulifanya vizuri zaidi.


8. Rama Dee > Nikki wa Pili

Tayari Nikki wa Pili alikuwa ameshasikika kwenye wimbo ‘Niaje Nivipi’ alioshirikishwa na kaka yake, Joh Makini aliyekuwa akitamba wakati huo na kundi la River Camp Soldiers.


Ila bado Nikki alikuwa hajasikika yeye binafsi, ndipo alipotoa ngoma yake iitwayo ‘Good Boy’ akimshirikisha mkali wa RnB, Rama Dee ambayo ilimtambulisha na kumuongezea mashabiki.


9. Tundaman > Dogo Janja

Kilikuwa ni kipaji kipya ndani ya Tip Top Connection kwa wakati huo, ambapo Dogo Janja alikuwa chalii mdogo tena mwanafunzi wa shule ya msingi ila mwenye uwezo mkubwa wa kuchana.


Alimshirikisha Tundaman kwenye wimbo wake ‘Anajua’ ambao alikuwepo pia na Madee, ndio ulimtambulisha kwenye muziki wa Bongofleva na mengine yakabaki kuwa historia.


10. Ommy Dimpoz > Vanessa Mdee

Ingwa tayari Vanessa alikuwa ameshasikika kwenye baadhi ya ngoma kama ‘Money’ yake AY na ‘Press Play’ ya DJ Choka, bado mashabiki wengi walikuwa hawajamuelewa sana.


Hakuna ubishi kuwa wimbo ‘You and Me’ alioshirikishwa na Ommy Dimpoz ulimpa jina kubwa kwenye muziki wa Bongofleva, ndipo akaja kutoa wimbo wa kwanza alioupa jina la ‘Closer’.


©Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad