MAPEMA tu kabla hata dirisha la usajili halijafunguliwa, tayari Kamati ya Usajili ya Yanga, inayoongozwa na kaimu wake, Eng. Hersi Said, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, imevurugika kutokana na baaadhi ya wajumbe kulalamikia kutoshirikishwa kwenye usajili wa Ibrahim Ajibu.
Ajibu aliwahi kuitumikia Yanga msimu wa 2018/19, akitokea Simba na kuisaidia kumaliza katika nafasi ya pili kabla ya kurejea upya Simba ambapo hakuonyesha uwezo mkubwa kama aliokuwa nao, jambo lililowafanya sasa kumsajili tena.
Chanzo chetu kutoka ndani ya Yanga kimeeleza kwamba, pamoja na kamati hiyo kukamilisha usajili wa Ajibu, mambo yametibuka vibaya, ambapo baadhi ya wajumbe wamelalamika kutoshirikishwa kwenye usajili huo huku wakihoji dhumuni la kumrejesha kwake Yanga.
“Wale kamati ya usajili kwa sasa wanajifanya wana siri sana lakini siri zao nadhani sasa zimeanza kuwapeleka kubaya, kwani usajili wa Ajibu umetibua hali ya hewa kwenye kamati hiyo baada ya mjumbe mmoja kumsajili bila kuwashirikisha wenzake.“
Ni kweli Ajibu tayari amesajili kwetu kwa mkataba wa miaka mitatu, ila vurugu kubwa ni kwamba wajumbe wanahoji kwa nini usajili wake haukuwa na majadiliano kama ilivyo kwa wachezaji wengine, jambo ambalo majibu yake yameleta vurugu kubwa kiasi cha wengi kuhoji usajili huo utaisaidia nini timu,” kilisema chanzo hicho.
Championi lilimtafuta Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli hakuweza kupokea simu yake huku Afisa Mhamasishaji wake Antonio Nugaz yeye alisema yupo kwenye kikao atafutwe baadaye