Askofu wa Dayosisi ya Munich na Freising nchini Ujerumani, Kadinali Reinhard Marx, ameomba kujiuzulu katika barua aliyomwandikia kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.
Kadinali huyo ameeleza katika barua hiyo kwamba madhumuni yake ni kukubali wajibu juu ya kashfa ya udhalilishaji wa kingono uliofanywa na baadhi ya viongozi wa kanisa, aliyoiita kuwa ni maafa.
Kadinali Marx ameeleza kuwa taarifa na uchunguzi wa kipindi cha miaka 10 iliyopita umebainisha kushindwa kwa watu binafsi na makosa ya kitaasisi. Katika maelezo yake kwa vyombo vya habari, Dayosisi Kuu ya Munich na Freising imesema Papa Francis amemtaka Kadinali Marx aendelee na wadhifa wake hadi hapo Baba Mtakatifu atakapomjibu.
Uchunguzi ulioidhinishwa na Baraza la Maaskofu la Ujerumani na kuchapishwa mwaka 2018 ulionesha kwamba viongozi wa kanisa 1,670 waliwadhalilisha kingono watoto zaidi ya 3,600 kutoka mwaka 1946 hadi mwaka 2014.