Beki wa AS Vita alamba saini ya miaka miwili Yanga



SASA ni rasmi Yanga imemsainisha beki wa kulia wa AS Vita na timu ya taifa ya DR Congo, Shaaban Djuma kwa mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuitumikia klabu hiyo.

Djuma Shaaban unakuwa ni usajili wa kwanza wa Yanga wa kimataifa ambapo klabu hiyo imelenga kukiboresha kikosi chao kuelekea msimu ujao ambapo timu hiyo ina nafasi kubwa ya kushiriki michuano ya kimataifa.


Yanga chini ya mwenyekiti msaidizi wa kamati ya usajili, Eng. Hersi Said, imesema kuwa timu hiyo itafanya usajili wa maana kwa ajili ya kufanya vizuri kwa msimu ujao katika mashindano yote ambayo watashiriki.


 Meneja Mkuu wa AS Vita, Yves Dida Ilunga, alikiri wazi kuwa Klabu ya Yanga tayari imekamilisha usajili wa beki huyo na hivi karibuni watatangaza dili hilo.


“Kila kitu kimekamilika, Yanga imeshakamilisha taratibu zote za kumsajili Djuma, nadhani hivi karibuni kila kitu kitakuwa wazi juu ya dili la beki huyu, tunasubiri taratibu tu za timu ila kila kitu kimemalizika,” alisema meneja huyo.


Kwa upande wa meneja wa mchezaji huyo, Faustino Mukandila, yeye alisema: “Yanga imefanikiwa kumsajili mteja wangu, Shaaban Djuma, hivyo itoshe watu wafahamu kuwa kila kitu kimekamilika siku siyo nyingi tutangaza dili hilo kuwa lipo tayari.”


Naye nahodha wa Klabu ya AS Vita na timu ya taifa ya Congo, Jeremy Mumbere, alifunguka juu ya dili la nahodha mwenzake wa klabu hiyo Shaaban Djuma kujiunga na Yanga.


“Tayari Djuma amekamilisha usajili wake wa kujiunga na Yanga, mimi tayari ameniaga kuwa atajiunga na Yanga mara baada ya kumalizika kwa mchezo wetu wa mwisho wa ligi tutakaocheza Juni 6 (Jumapili).


“Ameniambia kuwa amesaini mkataba na Yanga wa miaka miwili, hivyo baada ya mchezo wa mwisho ataanza mipango ya safari ya kuja Tanzania kwa ajili ya kukamilisha usajili wake,” alisema nahodha huyo wa AS Vita.


Naye Djuma mwenyewe tulipomtafuta kuzungumza kuhusu usajili wake wa kujiunga na Yanga, alisema: “Nafikiri taratibu zilizobaki ni kwa upande wa Klabu ya Yanga na AS Vita kuweka wazi dili hili, nachofahamu kila kitu kimekamilika, nasubiri wao waweke wazi ishu hii ili kila mtu afahamu kinachoendelea.


Tulipomtafuta Makamu Mwenyekiti Kamati ya Usajili ndani ya Yanga, Eng.Hersi Saidi kuzungumzia juu ya usajili wa beki huyo simu zake ziliita bila majibu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad