BODI ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia imeidhinisha mikopo minne yenye masharti nafuu yenye jumla ya dola za Marekani bilioni 1.017 (sawa na shilingi trilioni 2.3391) kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma jana Juni 6.
Dkt. Nchemba alisema kuwa miradi iliyopata idhini ya Bodi hiyo ni mradi wa kuboresha barabara za vijijini (RISE) wenye mkopo wa dola za Marekani milioni 300 na mradi wa kuimarisha mazingira ya ufundishaji na mafunzo katika taasisi za elimu ya juu (HEET) wenye mkopo wa dola za Marekani milioni 425.
“Miradi mingine ni mradi wa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao (DTP) wenye mkopo wa dola za Marekani milioni 150 na Mradi wa kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma bora za umeme visiwani Zanzibar wenye mkopo wa dola za Marekani milioni 142,” alisema Dkt. Nchemba.
Alieleza kuwa mradi wa kuboresha barabara za vijijini utahusisha ujenzi wa jumla ya kilomita 535 kwa kiwango cha lami katika wilaya sita za mikoa ya Iringa, Lindi, Geita na Tanga na ukarabati wa maeneo korofi ya barabara za vijijini nchi nzima.
Alisema kuwa mradi wa kuimarisha elimu ya juu utaimarisha mazingira ya ufundishaji katika Taasisi za Elimu ya Juu katika fani za kipaumbele cha Taifa, kupitia upya na kuboresha mitaala ya vyuo vikuu ili kuwa na wahitimu wanaoendana na soko la ajira na kuchangia maendeleo ya nchi na uchumi kwa ujumla.