Mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) amewafutia shtaka la utakatishaji fedha wakurugenzi wa kampuni ya kuagiza vinywaji vikali nchini, Bevco Limited na sasa wako huru kuomba dhamana.
Mapema wakili wa serikali, Ester Martin amedai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya kuwa leo Juni 24, 2021 kesi hiyo ya uhujumu uchumi imekuja kwa ajili ya kuifanyia mabadiriko hati ya mashtaka kwa kuondoa shtaka moja la utakatishaji fedha na kuwasomea washtakiwa mashtaka yaliyobaki.
Katika kesi mpya washtakiwa wanakabiliwa na makosa 48. Lipo shtaka moja la kuongoza genge la uhalifu, mashtaka matano ya kushindwa kulipa kodi, mashtaka saba ya kughushi, mashtaka saba ya kutoa nyaraka za uongo, mashtaka 14 ya kukwepa kodi na shtaka moja la kusababisha hasara kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zaidi ya Sh bilioni 1.6.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Melaine Philipe na Thierry Lefeuvre raia wa Ufaransa, Joseph Rwegasila aliyekuwa Diwani wa Makongo na Mwanasheria Ntemi Massanja.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Septemba Mosi mwaka 2017 hadi Septemba 2020
Washtakiwa wanadaiwa kwamba kati ya Oktoba mwaka 2017 hadi Juni mwaka 2020 jijini Dar es Salaam, waliisababishia TRA kupata hasara ya Sh 1,658,370,376.29. na kesi imeahirishwa hadi Julia 6, mwaka huu.