MBUNGE wa Arusha Mjini, Mrisho Mashaka gambo ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya ukaguzi wa Hifadhi zote za Taifa na kupeleka ripoti bungeni kuhusu watalii wanaotembelea kila hifandi na kiasi cha pesa kinachoingizwa na kila hihadhi kutokana na utalii huo.
Gambo amesema hayo leo Ijumaa, Juni 4, 2021, wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bungeni jijini Dodoma huku akiitaja Hifadhi ya Burigi Chato iliyopandishwa hadhi na Hayati Dkt. John Magufuli kuwa hifadhi ya taifa.
“Kwenye taarifa ya Waziri anasema hapa kuwa utalii unachangia pato la taifa kwa asilimia 17 na fedha za kigeni kwa asilimia 25, mimi nadhani taarifa ya Waziri ni ya zamani sana kwa namna ambavyo janga la corona limeathiri sekta ya utalii nchini na duniani kote.
“Ukiangali taarifa yake amesema hadi Aprili mwaka 2019 target ilikuwa kukusanya Tsh bil 584 na sisi tumekusana Tsh bil 89 ambayo ni sawa na asilimia 15 tu.
“Mchango wa utalii kwa GDP umeshuka kutoka kutoka asilimia 17.5 mpaka asilimia 11.5 na bado wamepandisha tozo za utalii wakati nchi nyingine za Afrika Mashariki zimeshusha. Dunia nzima inatoa ahuweni kwenye utalii lakini sisi tunaongeza gharama Mimi naona bado kuna kazi ya kufanya.
“Ninashauri tupitie hifadhi zote za Taifa especially ya Burigi Chato, mlete hapa mtuambie imepokea wageni wangapi na imeingiza kiasi gani na inatumia gharama kiasi gani kuendeshwa, sio tunaanzisha hifadhi nyingi na gharama za uendeshaji zinakuwa kubwa kwa sababu utapeleka watumishi kule utawalipa, gharama hizi unakuwa mzigo kwa mtalii ndio maana tunapandisha tozo kila mara.
“jambo jingine, ukienda Kenya, kupima corona ni dola 30 kwa hospitali za Serikali na dola 50 kwa hospitali private lakini hapa kwetu ni dola 100, sasa najiuliza kwani corona nayo ni fursa? Kituo cha kupimia corona (maabara) tuncho kimoja tu. Hili jambo inabidi tuliangalie upya,” amesema Mrisho Gambo.