KUELEKEA mchezo wao wa dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba utakaopigwa siku ya Jumamosi, Uongozi wa kikosi cha klabu ya Yanga umefunguka kuwa hauna presha na mchezo huo, na wanaamini kwa maandalizi wanayoyafanya wataibuka na ushindi.
Yanga Jumamosi hii watakuwa wageni wa Simba katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam. Mchezo huu hapo awali ulipangwa kupigwa Mei 8, kabla ya kuahilishwa mpaka Julai 3, mwaka huu.
Timu hizo zinaingia katika mchezo huu zikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1, iliyopatikana katika Mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Novemba 7, mwaka jana.
Akizungumzia maandalizi yao, Ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema: “Baada ya kufanikiwa kufika hatua ya fainali ya kombe la Shirikisho, kikosi chetu kimeendelea kuwa kambini kwa ajili ya kujiandaa na michezo yetu iliyosalia ya Ligi Kuu Bara ikiwemo mchezo dhidi ya Simba.
“Kwetu hatuna presha yoyote kuelekea mchezo huu, kwa kuwa tunautazama kama mchezo wa kawaida ambao tunakwenda kushinda na kuongeza pointi tatu muhimu, ”