Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa Yanga kupitisha rasimu ya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo aligeuka kivutio kwa hotuba na simulizi zake zilizojaa mzaha na masikhara.
Mh. Kikwete aligeuka kivutio kikubwa kwenye hotuba yake pamoja na kuikumbusha klabu yake pendwa maarufu kama ‘wananchi’ kufanya usajili mzuri kwa wachezaji wenye hadhi pamoja na kuvumilia makocha, lakini hakuacha kuchomekea imani za kishirikina katika timu hiyo miaka ya nyuma.
Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa DYCC uliyopo Temeke na kufungiliwa rasmi saa 4:00 asubuhi ,ulikuwa na ajenda kadhaa zinazolenga kuijenga upya klabu, japo ile yenye nguvu ilikuwa kubariki mchakato wa mabadiliko ya klabu kwenda kwenye mfumo wa uwekezaji.
Pia wajumbe wa mkutano mkuu walionekana kufurahishwa zaidi na uwakilishwaji wa mpango wa ujenzi wa makazi ya wachezaji na viwanja vya kuchezea kule Kigamboni.