MFALME Ali Saleh Kiba ‘AliKiba’ Juni 10 ameachia ngoma mpya inayokwenda kwa jina la Ndombolo. Mpaka sasa imefanya vizuri, ina wafuasi wasiopungua 541,207 huu ni mwendo mzuri.
Nimeandika makala haya lengo ni kumkumbusha Kiba kwamba, kama ni gari ndio kwanza limewaka.
Asiwaangushe mashabiki wake maana wanamuamini. Wamemuunga mkono kwa zaidi ya miaka 15 sasa tangu aanze muziki.
Anatakiwa kuonesha kweli ukongwe wake.Mara kadhaa amekuwa akipotea kwenye kilele cha mafahari wa Bongo Fleva. Anawaachia vijana, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na wakati mwingine hata Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’.
Unajiuliza, kweli Kiba anashushwa hadi daraja la nne au la tano na hawa vijana? Mbona anaujua muziki? Mbona anao uwezo mkubwa tu.
Usisahau, anao pia uzoefu wa kutosha. Kama ni fitna za muziki anazijua, kama ni baishara ya muziki anaifahamu vyema.Miaka kadhaa iliyopita, Kiba alipotea kwenye gemu kwa muda mrefu.
Aliporudi na kuachia ngoma kadhaa kali ikiwemo Cheketua, alifanya vizuri na watu wakaamini kweli mwenye kiti chake amerudi kama yeye mwenyewe alivyojinasibu.
Ngoma zake hizo mpya zilikamata, zikapigwa sana lakini hata hivyo hakufanikiwa kumtoa kwenye reli kijana wake Diamond ambaye wakati huo alikuwa ‘fire’. Akajikuta anafanya muziki wake lakini haufikii levo za Diamond.Miaka ikazidi kukatika, kila tukimsubiri Kiba arudi kwenye nafasi yake inashindikana.
Diamond akazidi kujiowekea mizizi kwenye muziki, akaendelea kuzalisha vijana ambao kwa namna moja au nyingine, wakageuka kuwa ndio wapinzani wa Kiba na si Diamond tena.
Kuna wakati Harmonize aliweza kumdhibiti vizuri tu Kiba na akawa hafurukuti. Yani unamuona kabisa mpinzani wa Diamond wa Harmonize.
Harmonize alipoondoka Wasafi Classic Baby (WCB), alijitutumua kwelikweli kuhakikisha anakuwa mpinzani wa Diamond.Kwa kiasi fulani alifanikiwa na hapana shaka hata Diamond hilo lilimuumiza kichwa. Alikaa chini na kuona ili kumkabili Harmonize, anatakiwa kuzidi kujitanua.
Akawekeza nguvu kubwa kwenye kuwakuza wasanii wake akiwemo Zuhura Othuman ‘Zuchu’ na Rayvanny.Zuchu akaongeza kasi na akawa mkubwa sana ndani ya muda mfupi. Huo ukawa ni wigo mwingine wa Harmonize kuweza kushindana. Harmonize akamjibu kwa kumsajili mwanamke kwenye lebo yake, Anjella.
Hii ilimfikirisha tena Diamond akaona kijana anapambana na ndipo alipoamua kumtoa Rayvanny ambaye alikwenda kuanzisha lebo yake.
Wakati wote huu, Kiba alikuwa hazungumzwi tena. Ulimwengu wa burudani ukawa unawazungumza zaidi Wasafi na Konde Gang.Unawazungumza zaidi Rayvanny, Diamond na Harmonize. Kiba wakati huo yupo tu, hatujui anafanya nini wakati naye ni msanii mkubwa.
Hapa ndipo kwenye msingi wa makala yangu, Kiba anatakiwa kujitathimini sana.Ajue kwamba anatakiwa kuwepo kwenye nafasi yake kimuziki.
Yeye anajua, ni fundi kwa nini akubali vijana hawa wamshike sharubu mara kwa mara? Ametoa wimbo wake mzuri wa Ndombolo na mashabiki wamemuunga mkono.Wimbo unachezeka, tunaona jinsi ambavyo ameanza kuachia vipande vya video akifanya mazoezi ya video ya wimbo huo. Video isichelewe sana sasa, afanye vitna ili wimbo huo uwe mkubwa.
Siwezi kusema afanye nini lakini yeye anafahamu muziki unataka nini.Ngoma ipo nafasi ya saba kwenye trending kwa sasa, kwa nini isifike namba moja kama ambavyo wenzake huwa wanafanya na ngoma inafika kwenye namba moja. Imekuwa ni kawaida tu pale Harmonize anapotoa ngoma, inafika namba moja.
Vilevile kwa Zuchu, Diamond au Rayvanny wakitoa ngoma zao lazima zifike kwenye namba moja trending.
Kwa nini Kiba na wewe usifike kwenye namba moja? Kiba anatakiwa kuchangamka. Anatakiwa kufanya kinachotakiwa kufanyika ili mambo yake yawe juu.Ndombolo imeshika hatamu, kanyagia hapohapo. Usikubali kushuka tena, unatakiwa kwenda juu.
Kupanga ni kuchagua, kama utaendelea kufanya maringo, kama utaendelea kufanya ule muziki wako wa mazoea badi utawaruhusu vijana watawale.Baada ya muda tutakusahau, tutaanza kuwajadili walewale ambao kila siku wanajadiliwa kwenye ulimwengu wa muziki. Kinachosikitisha zaidi, kina Zuchu au Nandy ambao wamekukuta kwenye gemu eti nao huwa kuna wakati wanazungumzwa zaidi kuliko wewe!
MAKALA Erick Evarist Erick Evarist