By Bernard James
Ni nani aliruhusu Watanzania 64 wafanyiwe majaribio ya dawa ya Ukimwi ya Virodene kati ya mwaka 2000 na 2001 licha ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kutotoa kibali?
Je, Watanzania hawa walipewa taarifa sahihi na za kutosha kabla ya kuruhusu miili yao itumike katika majaribio hayo, ambayo matokeo yake hakuna ajuaye hadi leo? Ni nani anastahili kuwajibishwa kwa tukio hilo?
Haya ni baadhi ya maswali yanayodai majibu kuhusu Watanzania hao 64 ambao kati ya mwishoni mwa mwaka 2000 na mwaka 2001 walitafutwa, wakaorodheshwa na kuingizwa katika mpango wa majaribio ya dawa ya Ukimwi iliyoendeshwa nchini na kampuni ya Virodene Pharmaceutical (Pty) Limited ya Afrika Kusini.
Majaribio hayo kama ilivyo kwenye mwenendo wa kesi, yanadaiwa kufanyika katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) Lugalo na Kituo cha Afya cha Chadibwa, kinachomilikiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Omar Mahita, huku yakiacha machungu kwa waliofanyiwa utafiti huo.
Miaka 20 baada ya kufanyiwa majaribio, watu wanaodai kuathirika wameendelea kudai fidia bila mafanikio kutokana na madhara ya kimwili na kijamii waliyoyapata.
Wanadai matumizi ya miili yao kwa majaribio ambayo waligundua hayakuwa na kibali cha Serikali wala viwango vinavyokubalika kisayansi, ulikuwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na udhalilishaji.
ADVERTISEMENT
Ingawa Mahakama Kuu imeitupa kesi ya kikatiba waliyofungua mwaka 2014 wakiomba mahakama itamke kuwa majaribio yale yalikuwa kinyume cha ubinadamu, yamewadhalilisha na hayakufuata utaratibu wa kisheria, waathirika hao wameapa kuendelea kupigania haki yao.
Baadhi yao wanadai majaribio yale yaliwasababishia matatizo zaidi ya kiafya, yakiwamo ya ini na tumbo.
“Tunaomba taarifa hizi zimfikie Rais, tunatumai tutapata msaada kutoka kwake, hatua za kiutawala zifanyike, apitie hili jambo kwa undani wake na atusaidie,” anasema mmoja wa waathirika hao, Steven William Kimaro (62).
Licha ya kwamba maombi ya kufanya majaribio ya dawa ya Virodene P058 yalikwishakataliwa katika nchi kadhaa duniani, kampuni hiyo ilifanikiwa kupenya nchini kuendesha majaribio hayo.
Wakati Virodene ikifanyiwa majaribio Tanzania bila kibali cha NIMR, tayari ilikwishakataliwa Uingereza, Ujerumani na Afrika Kusini yenyewe.
Jitihada za watengenezaji wake kuanzisha majaribio nchini Afrika Kusini zilileta mtafaruku mkubwa mwaka 1997 kiasi cha dawa hiyo kusitishwa.
Virodene P058 ilitengenezwa na kemikali ya kiwandani ijulikanayo kama dimethylformamide au DMF. Watu walioiunga mkono dawa hiyo waliamini ingefanya maajabu makubwa katika kutibu Ukimwi, lakini wanasayansi walionya mapema kuwa ingeweza kufanya hali ya Ukimwi kuwa mbaya zaidi.
Dawa hiyo haikuwahi kujaribiwa kwa wanyama na ilipingwa na wanasayasi wakubwa wanaofanya utafiti wa dawa na chanjo ya Ukimwi.
Licha ya kupingwa, walioitengeneza, akiwamo mtaalamu wa dawa Michelle Olga Patricial Visser na aliyekuwa mume wake, mfanyabiashara Jacques Siegfied waliendelea kuandaa majaribio matatu ya Virodene kwa binadamu katika nchi tatu tofauti.
Hadi leo, waliofanyiwa majaribio ya chanjo hiyo Tanzania kati ya Machi 2000 na Septemba 2001 hawajui lolote kuhusu matokeo ya chanjo hiyo.
Julai 2001 aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Andrew Kitua alinukuliwa akisema majaribio hayo hayakuwahi kupata kibali cha taasisi yake, ingawa watengenezaji wake walidai yalifuata kiwango cha kimataifa cha maadili, sayansi na usalama wa majaribio ya dawa.
Yakataliwa Afrika Kusini
Wazalishaji wa Verodine walianzisha majaribio nchini Afrika Kusini, licha ya upinzani mkali kutoka kwa mamlaka za dawa za nchi hiyo, hata kabla dawa hiyo haijafanyiwa utafiti wa kutosha na kutolewa maoni tofauti na wanasayansi.
Baada ya kupitia taarifa (data) za majaribio hayo, mamlaka ya afya nchini Afrika Kusini ilitamka wazi kuwa hakukuwa na ushahidi wowote kuwa Verodene inafanya kazi.
Baadaye Baraza la Udhibiti wa Dawa Afrika Kusini, lilizuia majaribio ya ziada ya Virodene kwa binadamu, likisema dawa hiyo ilikuwa na uwezekano mkubwa wa kuleta madhara kwa binadamu na kwamba hakukuwa na chembe ya ushahidi kuwa ingefanya kazi.
Wasaka nchi nyingine
Wakati huohuo, matokeo ya utafiti mdogo yaliyochapishwa mwaka 1997 katika jarida la AIDS Research and Human Retroviruses na watafiti wa Chuo Kikuu cha Washington, yalionyesha kuwa DMF ingeweza kukuza zaidi tatizo la Ukimwi.
Kabla ya utata juu dawa hiyo haujaisha nchini Afrika Kusini, kina Visser walianza kutafuta nchi nyingine ya kufanyia majaribio. Kwanza, walianzia Uingereza ambayo haihitaji kibali cha mdhibiti wa serikali kwa tafiti za kiafya zinazofanywa kwa watu wanaojitolea kwa nia ya kujua usalama wa dawa.
Majaribio madogo ya Virodene yalifanyika London yakihusisha watu 15 ambao tayari walikuwa na maambukizi ya Ukimwi.
Matokeo ya utafiti huo uliofanyika kati ya mwishoni mwa 1998 na 1999 hayajawahi kuchapishwa, lakini ripoti ya ndani ya Bi Visser na Leonard Sequeira, mchunguzi mwenza wa majaribio ya Tanzania, ilihitimisha kuwa ‘Virodene patch’ moja ilivumilika kwa wajaribiwa, wakati nyingine mbili zilizotumika kwa pamoja zilisababisha maumivu ya tumbo na matatizo ya ini.
Verodine yaingia Tanzania
Baada ya Uingereza, kituo kilichofuata kwa majaribio ya Virodene kilikuwa Tanzania. Awali, pendekezo la kufanya majaribio ya binadamu Tanzania yalikataliwa na NIMR, baada ya kugundua matatizo makubwa ya ‘kimetholojia’ ya majaribio hayo yaliyohitaji kurekebishwa.
Hata hivyo, Bi Visser aliwahi kunukuliwa na jarida la Wall Street akidai kuwa tayari kampuni yake ilikwishawasiliana na majeshi ya ulinzi kufanya majaribio hayo kwa niaba yao.
Katika kesi waliyofungua mahakamani, waathirika wa utafiti huo nchini Tanzania, wanadai majaribio ya Virodene yalifanyika Dar es Salaam katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi, Lugalo na kituo cha afya Chadibwa.
Alipoulizwa na Mwananchi anafahamu nini kihusu utafiti huo na kituo chake kilihusika vipi, Mahita alimhoji mwandishi alikuwa anataka nini wakati anajua kesi iliyofunguliwa na waathirika ilikuwa imekwisha.
Alipoulizwa zaidi, Mahita alikiri kuwa kituo hicho ni mali yake na kuongeza kuwa wakati majaribio ya Virodene yakifanyika, alikuwa amekikodisha.
“Kama kesi ilikwisha sijui unataka nini. Chadibwa ni mali yangu lakini nilikwishakodisha kwa mtu wakati hilo suala (majaribio) likiendelea. Mimi sikushiriki ila nilimkodisha mtu,” alisema Mahita.
Alikataa kutoa maelezo zaidi akidai hakuwa tayari kuzungumza lolote nje ya mahakama. “Kitu chochote nje ya mahakama siwezi kuzungumza, waulize Lugalo,” aliongeza.
Juhudi za gazeti kumpata msemaji wa Jeshi la Wananchi hazikufanikiwa. Baadhi ya waliofanyiwa majaribio katika Kituo cha Chadibwa, wamelieleza Mwananchi kuwa walikuwa wakihudumiwa na madaktari kutoka kikosi kimoja cha jeshi.
Majaribio ya Virodene Tanzania yalihusisha watu ambao tayari walikuwa wameathirika na Ukimwi na yalifanyika katika hatua tano.
Bi Visser alilieleza jarida la Wall Street Journal kuwa alipata vibali vyote muhimu, na kuonyesha kutoka katika faili lake barua kutoka vyombo ya ulinzi na usalama na vyombo binafsi vilivyomruhusu kufanya hivyo.
Alionyesha pia kibali kilichoandikwa kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Afya wakati huo, Dk Aaron Chiduo. Lakini Dk Chiduo alinukuliwa akisema kuwa aliwaelekeza watafiti na maofisa wa jeshi hao kupata kwanza kibali cha NIMR.
NIMR ilikataa kutoa kibali baada ya kuridhika kuwa utafiti huo haukukidhi viwango vya kimataifa.
Hata hivyo, Bi Visser anasema majaribio hayo yaliendelea kwa sababu walipata barua ‘nzuri’ kutoka kwa Dk Chiduo ambayo alidai ilisitisha maamuzi ya NIMR. Dk Chiduo hata hivyo, alikana kwa nguvu zote kuruhusu utafiti huo.
Kesho katika simulizi hii tutaona jinsi Watanzania waliotumika katika utafiti huo walivyopatikana na kilichoendelea katika wodi walizowekwa wakati wa majaribio