LISSU: Miezi 3 ya Samia kuna uhuru, watu wanapumua



MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Tundu Lissu, amesema kwa kipindi cha miezi mitatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, kuna uhuru, watu wanapumua na vyombo vya habari vinaandika vitu ambavyo vilikuwa haviwezi kuandika.

Lissu alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa na televisheni moja nchini Kenya.

“Ni kweli kuna mabadiliko, tuna rais mpya, Samia Suluhu Hassan. Katika miezi mitatu ambayo amekuwa rais, ni kweli kuna mambo yamefanyika ambayo yako tofauti na miaka mitano iliyopita. Kuna uhuru, watu wameweza kupumua, sasa hivi kila mtu anapumua, magazeti na vyombo vyetu vya habari sasa hivi vinaandika vitu ambavyo vilikuwa havidiriki kuandika,”alisema Lissu.

Akijibu swali aliloulizwa kuhusu uzuri wa marais wastaafu, Lissu alisema kwa kuanza na awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, yapo aliyoyafanya.

“Kizuri cha Mwalimu Nyerere, alijenga na alikuwa rais muda mrefu kuliko kiongozi mwingine yeyote, alikaa madarakani miaka 24, lakini pamoja na kukaa muda mrefu madarakani, aliachia kwa hiari na bila kuhusishwa na wizi au ufisadi au uchafuzi wa mali za umma,” alisema na kuendelea:


 
“Aliondoka madarakani akiwa na mikono misafi, akiwa msafi kwenye masuala ya matumizi ya madaraka na mali za umma, huwezi kumtuhumu Mwalimu Nyerere kwamba alituibia, hakutuibia.”

Kuhusu Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Lissu alisema aliirudisha nchi katika msingi mzuri uliosaidia kuokoa uchumi na pia ndiye aliyeleta mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Kuhus Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa, Lissu alisema hakuvuruga mfumo wa vyama vingi na alidhibiti Idara ya Usalama wa Taifa kwa kuitungia sheria ya kudhibiti mamlaka yake.


Kuhusu Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Lissu alisema miaka 10 ya Kikwete itakumbukwa kwa kuimarisha Bunge, kuweka bunge hilo kuwa mubashara na alipanua demokrasia.

“Na katika kipindi hiki ndipo tuliona jinsi ambavyo bunge linaweza kuwa, lakini ni rais ambaye chini yake demokrasia ilipanuka, vyama vya upinzani kama CHADEMA vilipata nguvu kubwa sana,” alisema Lissu.

KATIBA MPYA

Akizungumzia kuhusu vuguvugu lakudai Katiba mpya linalofanywa na chama chake, Lissu alisema hakuna namna yoyote ambayo chama kikuu cha upinzani kitaenda kwenye uchaguzi na Tume ya Taifa ya Uchagu (NEC) kama ilivyo kwa sasa.

WANACHAMA 19

Akizungumzia waliokuwa wanachama chake wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama chake (BAWACHA), Halima Mdee na wenzake 18, Lisssu alisema anashangaa sababu za watu hao kuendelea kuwapo bungeni wakati chama chao kilishawafukuza uanachama.

“Hawa 19 wanaoitwa wabunge, tumewafukuza uanachama, wako bungeni kwa nini, ili uwe mbunge au diwani au hata mwenyekiti wa kijiji au mtaa, lazima uwe mwanachama wa chama cha siasa na ukipoteza uanachama kwa mujibu Katiba,
unapopoteza ubunge au udiwani  automatic, hawa tumewafukuza kwenye chama, wako bungeni kwa  nini?” alihoji Lissu.

“Na hili ni suala muhimu sana, kuna makosa makubwa ya jinai yamefanyika, kuna watu wamegushi nyaraka za kuwafanya hawa watu wawe wabunge, sheria ya uchaguzi ya  Tanzania inasema hivi, ili mtu awe mbunge wa viti maalum anayewakilisha wanawake, lazima kwanza chama chake kipeleke majina ya hao walioteuliwa kuwa wabunge kwa NEC,” alieleza na kuongeza:

“Sisi hatujawahi kupeleka jina hata moja kwa sababu tulijadiliana kwenye kamati kuu ya chama, tukasema kwamba hatukubaliani na uchaguzi, na hatutapeleka majina ya wabunge na hatutachukua pesa ya ruzuku .”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad