Na Ahmad Mmow, Nachingwea.
Mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema muundo uliopo sasa unaosababisha kila kitu kufanywa na serikali kuu kwaniaba ya wananchi haufai na unazorotesha maendeleo.
Mbowe ameyasema hayo leo mjini Nachingwea alipozungumza na wanachama na viongozi wa CHADEMA wa wilaya ya Nachingwea na mkoa wa Lindi. Ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake katika kanda ya Kusini inayounganisha mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.
Alisema miongoni mwa sababu zinazo sababisha nchi kushindwa kwenda kwa kasi kubwa kimaendeleo ni muundo na mfumo wa sasa wa utawala ambao umetoa uwezo kwa serikali kuu kuamua na kupanga kila kitu kinachowahusu wananchi. Muundo ambao aliuita ni wa watu wachache kupanga na kuamua hatima ya maisha ya wengi.
Alisema kwakubaini muundo huo unakandamiza uhuru wa walio wengi kupanga na kuamua hatima ya maisha yao kupitia raslimali na maliasili zilizopo katika maeneo yao, chama hicho kinaona njia nzuri na sahihi ni kuwapa wananchi madaraka na uwezo wa kupanga na kuamua hatima yao kupitia serikali za majimbo.
Alibainisha kwamba muundo wa sasa umesababisha pia kuwe na viongozi wasiochaguliwa na wananchi wanao waongoza. Hali inayosababisha viongozi hao aliowataja niwakuteuliwa kushindwa kuwaheshimu wananchi. Badala yake waziheshimu mamlaka za uteuzi zilizowateua.
'' Mu ametoka Kilimanjaro ameletwa Lindi. Hajui utamaduni, mila wala desturi za watu wa Lindi lakini ndiye anaeamua hatima ya korosho za Lindi, hakuchaguliwa hata kwa kura moja lakini ameletwa awa kontroo ( awadhibiti) wananchi. Anaweza kuja na askari polisi akamkamata hata mbunge wenu mliye mchagua,'' alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA alikwenda mbali kwakusema iwapo chama hicho kitapewa ridhaa ya kushika dola kitafuta nafasi za uongozi za ukuu wa wilaya na mikoa.
Kwani chama hicho kinaamini katika kuwapa madaraka na uwezo wa wananchi kupanga na kuamua mambo yanayowahusu na matumizi ya raslima na maliasili zilizopo katika maeneo yao.
Alisema muundo na mfumo huo umechangia kwakiasi kikubwa mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo ina utajiri mkubwa kuwa duni kimaendeleo.
'' Wananchi wa mikoa hii mmecheleweshwa kimaendeleo. Ingawa viongozi wa juu serikalini walitoka na wawetoka huku lakini hawana msaada kwenu. Kwani maamuzi yanafanywa na serikali kuu, nikutokanana sera mbovu. CHADEMA kikishika madaraka kitaimarisha serikali za mitaa na wananchi watakuwa na sauti na raslimali zao,'' alisisitiza Mbowe.
Mbali na hayo, alisema chama hicho hakitapokea ruzuku toka serikalini. Bali kitajiendesha kupitia nguvu za wanachama wake kupitia ada na michango mbalimbali iliyopo kwamujibu wa katiba na kanuni za chama hicho.
Alisema mpango wa kukusanya D na taarifa za wanachama kidigitali kitakusanya fedha nyingi ambazo zitatosha kugharamia chama katika ngazi zote.
Aliwaasa wanachama kutimiza wajibu wao wakulipa ada na michango ili kuepuka utegemezi.