Mbunge ataka Bunge kujadili mauaji ya wivu wa mapenzi



Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (CCM),  Munde Tambwe ameomba mwongozo wa Spika wa Bunge akitaka chombo hicho cha kutunga sheria kujadili ongezeko la mauaji ya wivu wa mapenzi.

Mbunge huyo ameomba mwongozo huo leo Ijumaa Juni 4,  2021 mara baada ya  kipindi cha maswali na majibu.

Munde amesema kuna ongezeko la mauaji ya wivu wa mapenzi siku za hivi karibuni akitoa mfano wa vifo vilivyotokea mkoani Ruvuma na Iringa.

Juni 2, 2021 katika Chuo Kikuu Iringa Prudence Patrick (22) mwanafunzi wa mwaka wa pili wa chuo hicho alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kumnyonga hadi kufa mpenzi wake, Petronia Mwanisawa ambaye pia ni mwanafunzi wa chuo hicho ikidaiwa sababu ni wivu wa mapenzi.

Huku akiwataka wabunge kulaani mauaji ya aina hiyo mbunge huyo amesema, “kumejengeka tabia ya mwanaume kumpiga mwanamke kuwa kawaida kabisa katika jamii yetu na jambo hili husababisha wanaume kuwaua wanawake kwa kipigo.”

Amesema hata wanawake wenye macho mekundu wamekuwa wakiuawa kwa kudhaniwa ni wachawi, “huwa najiuliza hivi hakuna wanaume wachawi.”


Hata hivyo, naibu Spika wa Bunge,  Dk Tulia Ackson amesema hoja hiyo ni muhimu na nzito lakini si jambo la dharura kujadiliwa bungeni kulingana na kanuni za chombo hicho.


“Niombe Serikali mjitahidi kwanza kuelimisha jamii, mnapotoa elimu kuhusu uhalifu na hili mliseme na wanaothibitika kufanya vitendo hivi wachukuliwe hatua ili mtu ajue akifanya kitendo hicho ni mwisho wa maisha yake pia,” amesema.


Dk Tulia amesema si vyema mtu kufanya jambo la ukatili na kuendelea kuwepo katika jamii, akitaka hatua kuchukuliwa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad