HIVI sasa kipa wa Yanga, Metacha Metacha hayupo kwenye hicho baada ya kusimamishwa kutokana na kuonyesha ishara isiyofaa kwa mashabiki wakati timu yake ikiwashinda Ruvu Shooting 3-2, kwenye Uwanja wa Mkapa juzi Alhamisi.
Metacha alionyesha ishara ya kidole chenye tafsiri mbaya kwa mashabiki, baada ya kuzomewa kwa madai kuwa alicheza chini ya kiwango na kupelekea kufungwa mabao ambayo mashabiki walitafsiri kama uzembe.
Wakati Metacha akikumbwa na kadhia hiyo mengi yanasemwa ikiwemo kuhusishwa kwenda Simba na mashabiki wakidhani kuwa hiyo ndiyo sababu ya kipa huyo kuruhusu mabao ya makusudi na kwamba haipendi klabu hiyo kwa sasa.
Sasa meneja wa kipa huyo, Jemedari Said amefunguka mambo mapya akidai kuwa siyo kwamba mteja wake huyo haipendi klabu hiyo kwani ingekuwa hivyo angeshaondoka tangu zamani kwa kuwa mpaka sasa hajamaliziwa fedha yake ya usajili.
Mbali na hilo Jemedari alikwenda mbali zaidi akisema Metacha alicheza nusu ya msimu akiwa hajalipwa hata fedha kidogo na bado aliipambania timu:
“Siyo kweli kuwa Metacha amefanya makosa ya kinidhamu kwa sababu haipendi Yanga na anataka kuondoka.“Kwani hadi sasa bado anawadai hela yake ya mwaka jana, mbali na hivyo alicheza nusu msimu akiwa hajalipwa fedha yoyote, hivyo hiki kinachotokea sasa hakihusiani kabisa na ishu za yeye kutajwa kuondoka Yanga.
”KUHUSU KUFUNGIWA NA YANGA
“Yanga wamefanya jambo nzuri sana kuchukua maamuzi mapema, kwa sababu baada ya mechi mimi nilizungumza na Metacha na nikamwambia wazi kuwa sijapenda alichokifanya na siyo kitendo cha kiungwana.
“Na nikamwambia wazi kuwa akae tayari kwa lolote kutoka Yanga, kwa sababu hawatoweza kuvumilia kwa kuwa mimi naifahamu Yanga tofauti na watu wanavyofikiria na kwa bahati nzuri Yanga wakachukua hatua,” alisema Jemedari.
METACHA AOMBA RADHI
Jana mchana kipa huyo kupitia ukurasa wake wa Instagram aliomba radhi kutokana na tukio hilo.Metacha aliandika; “Kwa niaba ya familia yangu, management yangu na mimi mwenyewe napenda kuchukua fursa hii kuomba msamaha kwa viongozi wa klabu yangu ya Yanga SC, wachezaji wenzangu, benchi la ufundi, mashabiki wa klabu ya Yanga, mamlaka za soka nchini na wadau wote wa soka ambao wamekwazika kwa kitendo nilichokifanya jana.
Nikiri hakikuwa kitendo cha kiungwana hivyo najutia makosa niliyoyafanya.
Mimi kama mchezaji wa Yanga na timu ya taifa napaswa kuwa mfano mzuri siku zote mbele za watoto na wanaotamani kuwa kama mimi na watu ambao walikuwepo kiwanjani au waliona mechi kupitia televisheni majumbani kwao. Natambua mchango na umuhimu wa mashabiki kwangu binafsi na kwa klabu hivyo kitendo kile hakikupaswa kutokea. Natanguliza shukrani.
Stori: Issa Liponda, Dar es Salaam