Mfungwa aikana rufaa yake, arudishwa gerezani



Mfungwa anayetumikia adhabu ya kifungo cha miaka saba jela, George Alex juzi alikana kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyoidhinisha hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni iliyomtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo.

Mfungwa huyo alifikishwa mahakamani hapo baada ya kupata wito wa mahakama hiyo akitakiwa kufika kwa ajili ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, iliyokuwa imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu, Dk. Gerald Ndika, Mwanausha Kwariko na Barke Sehel.

George baada ya kupanda kizimbani aliieleza mahakama kuwa yeye haitambui rufaa hiyo, kwani hajawahi kukata rufaa yoyote kupinga hukumu ya Mahakama Kuu.

Mfungwa huyo aliieleza Mahakama ya Rufani kuwa alikubali kuendelea kutumikia adhabu yake kama ilivyoamuriwa na Mahakama Kuu na akaiomba mahakama hiyo iiondoe mahakamani rufaa hiyo ili aendelee kutumikia na hatimaye kukamilisha adhabu yake.

Awali rufaa hiyo iliitwa na mrufani, George Alex alipanda kizimbani na wakili wa Serikali Deborah Mushi aliieleza mahakama kuwa alikuwa tayari kuendelea na usikilizwaji.

Hata hivyo, Jaji Ndika baada ya kupekua jalada hilo alimueleza mfungwa huyo kuwa hapakuwa na sababu za rufaa ndani ya jalada.

George alijibu alikata rufaa Mahakama Kuu ambayo ilimuamuru aendelee na adhabu yake, jambo alilokubaliana nalo na hakukata rufaa tena.

Baada ya jibu la mfungwa huyo, Wakili Mushi alidai hana pingamizi, na akaomba rufaa hiyo iondolewe mahakamani chini ya Kanuni ya 77(4) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za mwaka 2009.

Maombi hayo yalikubaliwa na mahakama hiyo ikaiondoa rufaa hiyo, kama mrufani alivyoomba na kuungwa mkono na upande wa Serikali.

Baada ya amri hiyo, mrufani George akarejeshwa mahabusu gerezani kuendelea na adhabu yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad