SERIKALI imesema miradi yote ya kimkakati iliyoachwa na hayati Dkt. John Magufuli inaendelea kutekelezwa katika chini Rais Samia Suluhu.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Juni 5, 2021 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kueleza utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Uchumi wetu ulikuwa tunakuwa kwa asilimia 6.9 lakini tumepata mtikisiko, hali ya ukuaji wa uchumi wetu imeshuka mpaka 4.7% sababu ya corona, Serikali inafanya jitihada kwenda mbele zaidi, matarajio ya baadaye ya serikali angalau tufikie asilimia 10 au zaidi.
“Mfumuko wa bei upo kwenye kiasi ambacho tumejipangia kwa maana ya asilimia 3 hadi 7, takwimu zinaonesha kwa sasa mfumuko ni asilimia 3.3. Tunayo akiba ya kutosha ya fedha za kigeni zitakazotuwezesha kununua bidhaa na huduma miezi 4.7.
“Miradi yetu yote inakwenda vizuri na utekelezaji unaendelea, licha ya kupitia katika hali ya mabadiliko ya uongozi lakini Serikali inaendelea kutekeleza miradi yote na iko kwenye hali nzuri. Tuna ujenzi wa reli SGR, Dar – Moro (Km kama 300), Moro – Makutupola Dodoma (Km 422), sasa hivi tumeanza kipande cha tano Isaka – Mwanza (Km 341) Serikali imeshatoa Tsh bil 372.3 kwa ajili ya kuanza kwa kazi za ujenzi.
“Ujenzi wa reli ya SGR, Dar – Moro kazi inaendelea tumefikia asilimia 91 wanakamilisha, Moro – Makutupola Dodoma wakandarasi wapo saiti na kazi imefikia asilimia 61. Matumaini yetu ni kwamba itakwisha kwa muda tuliyojipangia.
“Ujenzi wa mradi wa Umeme wa Bwawa la Nyerere (Megawatt 2115), kazi inakwenda vizuri wakandarasi wako saiti, mwezi machi tulikuwa tumefikia asilimia 45 na sasa mwezi Juni tumefikia asilimia 52, utekelezaji wake unaendelea vizuri.
“Kuhusu ununuzi wa ndege, tayari ndege 8 zimeshafika na ndege nyingine 3 zinaweza kufika muda wowote. Wote ni mashahidi mnaona Shirika la ATCL linavyofanya kazi nzuri, kwenye ndege hauhesabu mapato ya nauli tu, unahesabu na faida nyingine. Rais Samia ameshaagiza dosari ndogondogo za kiuendeshaji na utawala zifanyiwe kazi na zimeshaanza kufanyiwa kazi tayari.
“Tuna ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (kilometa 3.2) katika Ziwa Victoria, ni mradi mkubwa utagharimu Tsh bil 712 kukamilisha, ujenzi wake unaendelea na tumefikia asilimia 27, mkandarasi yupo saiti anaendelea na kazi.
“Dar es Salaam tuna ujenzi wa daraja la Tanzanite umefikia asilimia 77.19, Flyover ya Chang’ombe, Kurasini, barabara ya mwendokasi ipo asilimia 16, upanuzi wa barabara ya Morogoro, tunaamini Wizara ya Ujenzi itasimamia na kuharakisha.
“Tuna ujenzi wa meli ya MV Mwanza umefikia asilimia 74, nchi yetu mwaka huu ina mikataba 9 ya ujenzi wa meli. Watu wanaweza kusema mambo yamekwama baada ya mabadiliko ya uongozi, hapana, miradi inakwenda vziri. Mikopo ya wanafunzi kati ya Machi na sasa imetolewa takribani Tsh bilioni 213 ili wanafunzi wetu waendelee kusoma.
“Serikali imeendelea kugharimikia miradi ya maji mijini na vijijini, kwa kipindi hiki tangu Machi, Serikali imetoa Tsh bil 91, nishati Tsh bil 542, bomba la mafuta utekelezaji unaendelea na serikali imetoa Tsh bil 249.
“Mradi wa ujenzi wa reli Serikali imetoa Tsh bil 719 katika maeneo mbalimbali. Meli na Chelezo pale Mwanza imetoka Tsh bil 4, Tsh bil 129 katika sekta ya uchukuzi, hii ni kuazia Machi mpaka Juni.
“Ujenzi wa Barabara katika Mji wa Serikali Dodoma imepelekwa Tsh bil 17. Kwa ujumkla wake kwenye kipindi cha machi mpaka Juni, Serikali imetoa Tsh trilioni 2.6245 kwa ajili ya kuakikisha miradi hii inakwenda vizuri.
“Kuna mikataba ambayo imesainiwa na Taasisi na mashirika mbalimbali ya Kimataifa kiasi cha Tsh bil 845, mikataba mipya inayokuja ambayo iko karibu kusainiwa ni Tsh Tril 2.697, jumla Tsh Trilioni 3.5428.
“Kwenye sekta ya afya kuna kuajiri wafanyakazi 4000, ujenzi wa majengo, kununua vifaa tiba, magari 20 ya wagonjwa, Taasisi ya JKCI imeanza kufanya upasuaji wa ubongo bila kufungua kichwa tumepiga hatua kubwa sana kutoa huduma kwa wananchi,” amesema Msigwa.