Kabuga anazuiliwa The Hague nchini Uholanzi tangu Oktoba kufuatia kukamatwa kwake nchini Ufaransa mnamo MeiImage caption: Kabuga anazuiliwa The Hague nchini Uholanzi tangu Oktoba kufuatia kukamatwa kwake nchini Ufaransa mnamo Mei
Wakili wa Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Félicien Kabuga ameiomba mahakama ya kimataifa ya jinai (ICC) mjini The Hague kumpa muda zaidi ili kuandaa kesi kabla ya kuanza kusikilizwa kwa undani.
Kabuga anazuiliwa The Hague nchini Uholanzi tangu Oktoba kufuatia kukamatwa kwake nchini Ufaransa mnamo Mei 2020, kwa tuhuma za mauaji ya kimbari.
Kesi hiyo iliendelea tena Jumanne jioni, miezi sita baada ya kuahirishwa kwa ombi la pande zote mbili kujiandaa kwa kesi hiyo.
Jaji alitangaza Jumanne kwamba mahakama ilikataa ombi la Kabuga, mwenye umri wa miaka 86, la kuachiliwa kwa muda kwa sababu za kiafya. Mahakama imesema kuwa madai hayo hayana msingi kwa sababu afya yake inafuatiliwa kwa karibu.
Kesi hiyo iliendeshwa kwa njia ya video lakini Kabuga hakuonyeshwa kwenye picha hizo, lakini alisikika akijibu swali kwa lugha yake ya Kinyarwanda . Kabuga alisikika kwa sauti ya uzee na akionekana kuchoka.
Wakili wa Kabuga, Emmanuel Altit, alisema wanahitaji muda wa ziada kuandaa kesi yenye faili kubwa, kwani kuna maombi waliyowasilisha mahakamani ambayo hayajapatiwa majibu na kulikuwa na ugumu katika uchunguzi wao.
Alisisitiza kwamba upande wa utetezi bado unakabiliwa na tatizo la kulinda usalama wa mashahidi wao walioko nchini Rwanda na pia matatizo ya utendajikazi katika kipindi kigumu cha Covid 19.
"Upande wetu uko katika wakati mgumu wa kufanyia kazi, wakati upande wa mashitaka ulipata muda wa miaka mingi wa kujiandaa kwa kesi hiyo,sisi tuna shida ya kuwa na timu ndogo," alisema Altit.