Ole Sabaya Kitanzini, Tuhuma zazidi Kuongezeka

 


Moshi. Wakati aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akitarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mara ya pili keshokutwa, Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro imesema inachunguza tuhuma nyingine saba zinazomkabili.

Taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa imesema miongoni mwa tuhuma hizo ni ile iliyotolewa na mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, Elioth Lyimo aliyedai kuwa Sh25 milioni zake zilichukuliwa na Sabaya isivyo halali.

Jana mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Salum Hamduni akizungumza na gazeti hili alisisitiza kuwa ametuma vijana wake kuchunguza madai ya mfanyabiashara huyo kuporwa fedha zake na Sabaya baada ya taarifa zake kusambaa mitandaoni.

Katika maelezo yake kwa kina, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikesi alisema wapo baadhi ya watu wanatajwa kushirikiana na Sabaya kufanya uhalifu mkoani Kilimanjaro, akiwemo Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu ambaye naye anachunguzwa na endapo uchunguzi ukithibitisha kwamba alihusika atafikishwa mahakamani.

Juni 4, mwaka huu Sabaya (34) na walinzi wake watano walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali, likiwemo la uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kupokea rushwa.

Sabaya ambaye alisimamishwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei 13, 2021 kupisha uchunguzi alifikishwa mahakamani hapo akiwa amefungwa pingu huku waendesha mashtaka wakisema mtuhumiwa huyo na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo Januari 20 na Februari 9, mwaka huu.

Katika ufafanuzi wa tuhuma zao, Sabaya na wenzake watano anatuhumiwa kwa makosa ya kuunda genge la uhalifu, uhujumu uchumi, kujipatia fedha kwa njia ya rushwa na utakatishaji fedha ambapo Sabaya alijipatia Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara, Francis Mroso mkazi wa kwa Mromboo ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi ili amsaidie, jambo ambalo ni makosa kwa mujibu wa sheria.

Pia, Sabaya na walinzi wake wawili, Sylivester Nyengu (26) maarufu kicheche na Daniel Mbura (38) wanakabiliwa na makosa mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha wakidaiwa kuyatenda Februari 9, 2021.

Wanadaiwa walimfunga pingu na kumpiga Bakari Msangi, ambaye ni diwani wa CCM kata ya Sombetin na kumuibia Sh390,000 na pia katika eneo la Bondeni jijini Arusha wakitumia silaha, Sabaya na walinzi hao wanatuhumiwa kumpiga, kumtishia silaha na kumpora Ramadhani Ayoub simu na Sh35,000.

“Kama mlivyosikia kuna tuhuma mbalimbali zilikuwa zimeibuliwa kuhusu Sabaya, uchunguzi dhidi yake unaendelea katika Mkoa wa Kilimanjaro, ukikamilika na kuthibitisha tuhuma zinazomkabili atafikishwa mahakamani ili haki iweze kutendeka.

“Wote wanaotajwa kuwa walishirikiana naye uchunguzi unaendelea dhidi yao ili haki iweze kutendeka, ikiwa kuna mtu anatajwa kwamba alishirikiana naye katika kufanya uhalifu dhidi ya wananchi chunguzi zinaendelea dhidi yao na zitakapo kamilika na kuthibitishwa watafikishwa mahakamani,” alisema Wikesi huku akisema ni mapema mno kuanika wazi tuhuma hizo mpya za Sabaya.

Kuhusu Meya wa Manispaa ya Moshi ambaye pia ni diwani wa Kata ya Bomambuzi kutajwa kushirikiana na Sabaya, alisema uchunguzi unaendelea dhidi yake na ikithibitika alihusika atafikishwa mahakamani.

“Ni kweli Juma (Raibu) naye ametajwa, uchunguzi unaendelea kuhusiana na tuhuma anazotajwa nazo na endapo uchunguzi utathibitisha na yeye atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zake,” alisema Wikesi. Akimzungumzia mfanyabiashara Lyimo, Wikesi alisema ni kweli alifika katika ofisi yake na tayari ameshahojiwa na kwamba ushahidi unaendelea kukusanywa dhidi ya malalamiko yake na wanaendelea kupokea taarifa.

“Mfanyabiashara huyu tumeshamhoji na tayari ushahidi unaendelea kukusanywa na tunaendelea kupokea,” alisema Wikesi

Alichokisema Lyimo

Alipotafutwa mfanyabiashara huyo alikiri ni kweli alichukuliwa fedha hizo na Sabaya na kwamba vielelezo vyote ameshavipeleka Takukuru, ikiwemo taarifa za benki ambapo alitoa fedha hizo Februari 2, 2020.

“Ni kweli Sabaya alichukua fedha zangu Sh25 milioni na malipo ya benki kwa maana nilipofanya miamala Februari 2, mwaka jana ninazo tayari nimeshazipeleka Takukuru, kwa sasa siwezi zungumzia ilikuwaje kwa sababu taarifa zote kuhusu ilikuwaje nimeshazipeleka Takukuru,” alisema Lyimo.

Kauli bosi Takukuru

“Unajua kuna vyanzo vingi vya taarifa vya kufanyia kazi... taarifa hiyo (ya Lyimo kuchukuliwa fedha na Sabaya) mimi nilikutana nayo kwenye mitandao ya kijamii na nikaelekeza wasaidizi wangu walioko Arusha na Moshi wafuatilie na wamsikilize huyo mzee Lyimo,” alisema Hamduni


Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad