Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa ataenda kuangalia kwa undani sababu na vikwazo viliyopelekea hadi sasa kutoundwa kwa Baraza la Vijana la Kitaifa la kuwawezesha vijana kukutana na kuzungumzia changamoto zao zinazowakabili.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo mkoani Mwanza, kufuatia ombi la kuwepo kwa baraza hilo lililotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Nusrat Hanje, aliyeomba kwamba vijana wanatakiwa wawe na baraza litakalowakutanisha kujadili changamoto zao kwa pamoja na kuwasilishwa serikalini kwa kuwa wanazo changamoto nyingi ambazo haiwezekani kwa kijana mmoja mmoja kusimama na kuziongelea.
"Kama vijana bila kutazama jinsia zenu ama itikadi zenu za kisiasa na kidini mnakutana wapi kujadili mambo yenu na kuweka ajenda za kitaifa, na hapa linanikumbusha lile alilosema mwanangu (Nusrat) lile baraza la vijana ambalo limesemwa siku nyingi lakini halijaundwa, tutakwenda kuangalia kwa undani kwanini halikuundwa, kuna vikwazo gani na tuone jinsi ya kuwaundia jukwaa hilo," amesema Rais Samia.