Rais Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri wa Madini, Doto Biteko kukutana na wawekezaji katika sekta ya madini kujadili mfumo mzuri wa kuyalinda madini ya Tanzanite kwani madini hayo kwa sasa yamekuwa kama yanapatikana dunia nzima.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Madini Doto Biteko, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM mkoa wa Mwanza Antony Dialo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi pamoja na viongozi mbalimbali, akikata utepe kuzindua Kiwanda cha kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery Limited kilichopo Sabasaba mkoani Mwanza leo tarehe 13 Juni, 2021.
Akizungumza leo Juni 13, 2021 jijini Mwanza baada ya kuzindua kiwanda cha kusafisha madini, amesema ni madini yanayopatikana Tanzania tu, lakini hali inavyokwenda sasa ni kama yanachimbwa dunia nzima.
“Tanzanite ni madini ambayo Mungu ameipendelea Tanzania lakini sasa hivi nchi mbalimbali ukienda utayakuta. Hili ni zao pekee la madini tunaloweza kujivunia kama Watanzania, kuna haja ya kukaa kuipa jina itakayoipa upekee Tanzanite yetu, kuwa na mfumo wa kuidhibiti Tanzanite yote itakayochimbwa nchini inunuliwe na mashirika yanayohusika,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amemsisitiza Waziri Biteko na wawekezaji kuhakikisha wanaipandisha hadhi Tanzanite na kurekebisha mauzo yake kwenye soko la Dunia.