Siku za nyuma Rais Kenyatta alishutumiwa kwa kutoheshimu maagizo ya mahakamaImage caption: Siku za nyuma Rais Kenyatta alishutumiwa kwa kutoheshimu maagizo ya mahakama
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekosolewa kwa kukataa kuidhinisha uteuzi wa majaji sita.
Majaji hao sita ni miongoni mwa majaji 41 ambao walikuwa wamependekezwa kwa ajili ya uteuzi na Tume ya Huduma za mahakama nchini humo (JSC) miaka miwili iliyopita . Mmoja wa majaji hao alifariki.
Rais Kenyatta amekataa mapendekezo ya JSC licha ya maagizo mawili ya mahakama yaliyomtaka kufanya hivyo.
Alhamisi hii, rais ameidhinisha uteuzi wa majaji 34 na kuwaacha sita- wakiwemo majaji wawili ambao walikuwa miongoni mwa majaji watano ambao hivi karibuni walitangaza kuwa mchakato wa kufanyia marekebisho ya katiba (BBI) ulikiuka katiba.
Wataalamu wa sheria nchini Kenya wanasema rais hawezi kubadili orodha ya majaji walioteuliwa au mapendekezo ya JSC na hana chaguo ila kuwaidhinisha majaji wote walioteuliwa na tume hiyo
Hivi karibuni Bw Kenyatta aliishutumu mahakama kwa "kuvijaribu vikomo vya katiba" baada ya mahakama ya juu nchini hukmo kuzuia mpango wa serikali wa kufanya marekebisho ya katiba.