Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewakamata watu wawili wanaodaiwa kushirikiana na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kufanya vitendo vya kihalifu katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, Arterio Kawonga hatua hiyo imefikiwa kutokana na uchunguzi unaendelea dhidi ya Sabaya unaofanywa na maafisa kutoka makao makuu ya taasisi hiyo.
Kawonga alisema kuwa Takukuru itaendelea kuwapa taarifa wananchi kadiri uchunguzi huo utakavyokuwa unakamilika kwakuwa wanaendelea kufanyia kazi tuhuma mbalimbali zilizowasilishwa dhidi ya Sabaya na wenzake.
“Kuna kesi nyingine za kijinai ambazo zipo polisi na tayari kuna watuhumiwa wawili tuliwakabidhi polisi Mkoa wa Kilimanjaro, wengine ni walewale anaoshtakiwa nao Arusha aliofanya nao matukio katika wilaya za Hai na Moshi,” Kawonga anakaririwa.
Juni 4, 2021 Sabaya na wenzake wanaodaiwa kuwa walikuwa walinzi wake, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha, utakatishaji fedha, rushwa na kuongoza genge la uhalifu.
Rais Samia atoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya
Alifikishwa tena mahakamani Juni 18, 2021 ambapo Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka alisoma mashtaka yanayowakabili watuhumiwa hao. Pamoja na mambo mengine, Sabaya alidaiwa kuvamia duka la mfanyabiashara, Mohamed Saad lililopo mtaa wa Bondeni. Ilielezwa kuwa kwa kutumia silaha, waliwatishia na kuwalaza sakafuni watu waliokuwa eneo hilo akiwemo diwani wa Sombetini, kisha wakapora kiasi cha Sh. 900,000.
Katika tukio lingine la unyang’anyi, Sabaya na wenzake walidaiwa kuwa walitumia bunduki kumtishia na kumpora Ramadhani Khatibu kiasi cha Sh. 35,000 na simu ya mkononi aina ya Tecno.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni alisema kuwa wakati wanaendelea na uchunguzi dhidi ya Sabaya na wenzake, ndipo wanazidi kupata kubaini tuhuma nyingi zaidi dhidi yake.