Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MKURUGENZI wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Herbinder Seth, ameachiwa huru kwa masharti ya kutotakiwa kutenda kosa lolote kwa kipindi cha mwaka mmoja huku pia akitakiwa kulipa fidia ya sh. bilioni 26.9 kwa serikali.
Hatua hiyo imekuja baada ya Seth kuingia makubaliano na DPP ya kumaliza kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa inamkabili kwa njia muafaka.
Aidha Seth amekubali kuweka hati ya kiwanda cha kufua umeme cha IPTL chenye namba 45566 kiwanja namba 292/2 kilichopo Kunduchi salasala kama dhamana iwapo atashindwa kulipa fedha hizo.
Hata hivyo, mshtakiwa Seth ameshalipa kiasi cha sh. Milioni 200 na kiasi kilichobakia anatatakiwa kukilipa ndanj ya miezi kumi na mbili kuanzia leo Juni 16, 2021 na ameachiwa huru.
Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Wakili wa serikali Mkuu, Martenus Marandu aliieleza mahakama kuwa hana kumbukumbu zozote za makosa ya nyuma ya mshtakiwa ila ameiomba mahakama kutoa adhabu kulingana na kifungu cha sheria kinavyosema.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu za Huruma Shaidi amesema, ni wazi kwamba mshtakiwa ni mkosaji wa kwanza na amekubali kuingia makubaliano ili kufanya jambo hili liishe kwa njia muafaka kati yake na serikali ambayo haiumizi upande wowote ule.
" Ni wazi umekubali kulipa kiasi kikubwa cha fedha na unapaswa kulipa kwa kuzingatia makubaliano, umekaa mahabusu kwa muda mrefu, ni wazi umeona mengi na umejifunza mengi, kumepita maji mengi kwenye daraja lako lazima upewe adhabu itakayokuwezesha kutimiza mkataba kwa utaratibu uliowekwa na serikali. Amesema Shaidi.
"Mahakama inakuachia huru kwa masharti ( condition Discharge) usije ukatenda makosa tena kaa kipindi cha mwaka mmoja utakuwa chini ya uangalizi." Amesema Shaidi.
Kabla ya kusomewa adhabu hiyo, mshtakiwa Seth alisomewa upya mashtaka yake ambapo sasa ameshtakiwa na kosa moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuondolewa mashtaka mengine 11 ambayo yalikuwa yakimkabili yeye na mshtakiwa mwenzae James Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi mwenza wa IPTL.
Katika shtaka hilo jipya inadaiwa katika tarehe tofauti tofauti kati ya Novemba 29,2013 na Januari 2014 huko katika benki ya Stanbic Tawi la Kinondoni na benki ya biashara ya Mkombozi Tawi la St. Joseph ndani ya Manispaa ya Ilala jijini Dar ss is Salaam mshtakiwa alitenda kosa.
Imedaiwa siku hiyo kwa njia ya udanganyifu mshtakiwa alijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) USD 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27
Jopo la mawakili wanne wakiongozwa na wakili wa serikali Mkuu Martenus Marandu, wakili wa serikali Mkuu Renatus Mkude, wakili wa serikali Mwandamizi Wankyo Simon na wakili wa serikali Faraja Ngukah ndio waliendesha kesi hiyo.
Katika utetezi wake mshtakiwa Seth kupitia wakili wake Merkzedeck Lutema aliiomba mahakama kumpunguzia mshtakiwa adhabu yake kwani ni mkosaji wa kwanza na pia ana matatizo ya kiafya na amekaa mahabusu kwa a muda mrefu hivyo ameiomba mahakama kumpatia mteja wake adhabu kwa kuangalia muda aliokaa mahabusu.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Herbinder Seth akiwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu akisubili kusikilizwa kwa kesi yake.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme (IPTL), Herbinder Seth akitoka katika mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu mara baada ya kuachiwa huru kwa Masharti ya kutotend kosa lolote kwa kipindi cha mwaka mmoja.