Siri Nzito Mbowe, Zitto Kabwe Kugombana

 


Dar es Salaam. Imepita miaka minane tangu Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na wenzake walipofukuzwa Chadema kwa madai ya usaliti; sasa ameibuka na kusema ni kosa kubwa analolijutia mpaka leo.

Mbali na Zitto, wengine waliofukuzwa walikuwa Profesa Kitila Mkumbo ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Ubungo (CCM) na Waziri wa Viwanda na Biashara na kada Samson Mwigamba.

Watatu hao baadaye walianzisha chama cha ACT Wazalendo, lakini Profesa Kitila na Mwigamba walitimkia CCM mwaka 2017.

Akizungumza kupitia mtandao wa Nadj Media Center, katika Podcast ya ‘Speaking with Tundu Lissu, iliyorushwa hivi karibuni, Zitto alisema angetamani muda urudishwe ili asitende kosa hilo.

“Ni moja ya historia ambayo huwa inaniumiza mno kuliko kitu chochote katika historia ya kisiasa. Ni kitu ambacho nikifikiria huwa nasema kwamba ‘I wish ninge-undo this’ (natamani ningeirudisha nyuma historia) ili twende mbele, lakini ndiyo imetokea,” alisema Zitto katika mahojiano hayo.

Zitto, aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini na baadaye Kigoma Mjini tangu mwaka 2005 hadi 2020, alisema mpaka sasa haoni kitu kilichosababisha yeye na wenzake kufukuzwa Chadema.

Alisema kutokana na hali hiyo, aliwahi kukutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mwaka 2017 na kujadili suala hilo bila mafanikio.

“Mara ya mwisho nilikutana na Mbowe Dodoma. Katika mazungumzo yale tulikaa mpaka saa nane za usiku, hatukupata jibu. Tulikuwa pale Morena Hotel, hatukupata jibu tukasema tutakutana siku nyingine.

“Mpaka sasa hakuna kitu ninachoweza kushika nikasema hiki ndicho sababu ya kiwango kile ambacho ni irreconcilable (kutoafikiana) na mimi naamini kabisa kwamba tungeweza kupatana. Kilichotokea ndicho kimetokea, ni historia,” alisema.

Waraka wa mabadiliko 2013

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, aliyekuwa akiendesha mahojiano hayo alimuuliza Zitto kuhusu waraka waliouandaa, uliodaiwa kuandaa kufanya mapinduzi ya uongozi wa chama.

Akijibu swali hilo, Zitto, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa chama hicho kabla ya kufukuzwa, alisema waraka huo uligundulika kwenye kompyuta ya Samson Mwigamba ukimtaja lakini hakushiriki kuuandaa.

“Waraka ule niliusikia kwa mara ya kwanza, sikuwa nimeusikia. Mimi ningeweza kuwa mfaidika wa waraka ule, lakini sikuuona mpaka nilipoingia kwenye kamati kuu ya chama.

“Ni kweli ulikuwa unanielezea mimi, lakini katika yote ni kwamba haukuwa waraka unaokwenda kubadilisha uongozi wa chama kwenda kinyume na utaratibu na demokrasia ya chama,” alieleza Zitto.

Huku akijitenga na waraka huo, Zitto alisema haukulenga kupindua uongozi, kwani chama kilikuwa kikielekea kwenye uchaguzi wa ndani mwaka 2014.


“Kuita mapinduzi haikuwa sahihi, pili, sikuhusika, sikutia mkono wangu kwenye waraka ule na nilieleza kwenye kikao na tatu ninalokubaliana kwenye waraka ule ni waraka uliokuwa unatengeneza makundi kwenye chama,” alisema.

Akitegua fumbo la washiriki wa waraka huo waliotajwa kwa majina ya M1, M2, M3, Zitto alimtaja M2 kuwa ni Mwita Waitara ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

“M2 alikuwa Mwita Waitara kwa sababu tunatunza historia, hakutajwa pale kwa sababu ilibidi alindwe,” alisema.

Uchaguzi wa 2009

Kabla ya Zitto kufukuzwa Chadema mwaka 2013, fukuto lilianza katika uchaguzi wa chama hicho wa mwaka 2009 ambao Zitto alichukua fomu kupambana na Mbowe aliyekuwa akitetea kiti hicho.

Lakini sasa anasema anajutia hatua yake ya kugombea, kwa kuwa alishawishiwa na makundi ndani ya chama hicho.

“Kukubali kushawishika na kugombea lilikuwa ni kosa kubwa sana ambalo lilianza kuleta mgawanyiko ndani ya chama na naamini kwamba haukuwa uamuzi sahihi. Ni very big regret (ni majuto makubwa) ambayo ningerudishwa nyuma ninge undo that (ningerekebisha).”

Zitto anakumbuka jinsi walivyofanya kazi kubwa ya kukijenga chama hicho, ikiwa pamoja na operesheni Sangara iliyoongeza idadi ya wanachama.

“Ilitakiwa tuonyeshe umoja kwa ajili ya kuukabili uchaguzi uliokuwa unafuata wa 2010 kwa pamoja na kwenda mbele. Mimi naamini pale ndiyo makosa ambayo binafsi nilifanya na ninajuta, kwa kweli najuta,” anasema.

Mbali na uchaguzi wa Mwenyekiti, Zitto pia anakumbuka uchaguzi wa Baraza la Vijana (Bavicha) ambapo aliyekuwa akigombea uenyekiti alikuwa David Kafulila (sasa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu), ambaye naye alisimamishwa katika chama hicho, kisha akahamia NCCR Mageuzi.

Akifafanua zaidi jinsi kundi lililokuwa likimuunga mkono ndani ya chama lilivyomsukuma kugombea, Zitto anasema alijaribu kukwepa lawama kwa kutafuta ufadhili wa masomo nchini Ujerumani, lakini alilazimika kurudi nchini.

“David Kafulila aliniletea fomu airport. Nilisaini ile fomu pale airport. Picha iliyowekwa ilikwenda kutafutwa kwenye tovuti, sikwenda kupiga kwa ajili ya ile fomu. Lakini sasa lile kundi linalokuunga mkono inabidi kulilinda na wakati huo huo unaona unakosea.”

Zitto kikaangoni

Akieleza jinsi alivyoitwa na kamati kuu wakati wa uchaguzi huo, Zitto alisimulia jinsi marehemu Profesa Mwesiga Baregu alivyomkaripia.

“Nakumbuka alikuwepo Mzee Mtei (Edwin), marehemu (Philemon) Ndesamburo ambaye naye alitaka nigombee, alikuwapo Profesa Baregu ambaye alikuwa na msimamo wa kati na yeye ndiye aliyenikaripia kwenye kikao akisema: ‘Tatizo lako you are too arrogant (una kiburi sana), lazima u manage arrogance (udhibiti kiburi).”

Hata hivyo, alisema katika kikao hicho aliamua kujitoa kwenye kinyang’anyiro licha ya aliyekuwa Katibu Mkuu (Dk Wilbroad Slaa ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden, kushauri wakubaliane na Mbowe kuachiana vipindi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad