Siri Vita Wanaompinga Mondi Tuzo Za BET





JAMBO usililolijua ni kama usiku wa giza! Ndicho kinachoendelea sasa katika tasnia ya burudani baada ya mashabiki muziki nchini Tanzania, wanasiasa na watu wa kada mbalimbali kupata mhaho kuhusu kumuunga mkono msanii machachari Bongo na Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ katika Tuzo za BET bila kutambua kuwa hawana uwezo wa kumpigia kura, Gazeti la IJUMAA linachambua.

 

Tangu orodha ya wasanii walioteuliwa kuwania tuzo hizo za BET kutolewa Mei 27, mwaka huu, kumeibuka makundi mbalimbali yanayopinga Diamond Platnumz au Mondi kuungwa mkono kwa kupigiwa kura ili ashinde tuzo hiyo.

 

Katika orodha hiyo ambayo Diamond anawania kipengele cha Best International Act, Diamond ambaye ndiye msanii pekee kutoka Afrika Mashariki aliyepenya kwenye tuzo hizo, anachuana na wakali wenzake kama vile Wizkid na Burna Boy wa Nigeria, Emicida wa Brazil, Headie wa Uingereza, Aya Nakamura na Youssoupha wa Ufaransa na Young T na Bugsey wa Uingereza.



WANAOMPINGA MONDI

Hadi sasa waliojitokeza hadharani kumpinga Mondi ni baadhi ya wadau wa burudani akiwamo mtangazaji na mwigizaji wa Bongo Movies, Burton Mwamba ‘Mwijaku’ ambaye katika mitandao ya kijamii anashea link za akaunti za Instagram za Mtandao wa BET na Burna Boy na kuwataka watu kumpigia kura msanii huyo.

 

Msimamo wa Mwijaku ni kwamba anadai kuwa ni kheri kumpigia kura Burna Boy kutoka Nigeria kwa sababu anao uwezo wa kushinda kipengele hicho kuliko kumpigia Mondi.

 

Wakati kwa upande wa siasa, wanasiasa hususani wafuasi wa vyama vya upinzani wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Chadema (Bara), Tundu Lissu ambaye naye bila kutambua amekiri kuwa hatomuunga mkono Mondi kwa kuwa si mpigania haki.

 

Wafuasi hao wameenda mbele zaidi kwa madai kuwa Mondi amekuwa akishiriki kampeni za chama tawala (CCM), jambo ambalo wanaona ni kama usaliti kwao.

 

WANAOMUUNGA MKONO

Wanaomuunga mkono ni wengi na kampeni mbalimbali zinaendeshwa kwenye mitandao ya kijamii kuhamasisha Watanzania kumpigia kura Mondi bila kutambua kuwa hakuna uwezekano huo. Baadhi yao ni rapa mkongwe na aliyekuwa Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule ‘Profesa Jay ’ ambaye ametolea mfano namna alivyokosa tuzo za MTV Base kwa kukosa kura za kutosha kutoka kwa Watanzania.Wengine ni wabunge ambao katika mijadala mbalimbali ndani ya Bunge nao pia wameingia kwenye mkumbo wa kuhamasisha Watanzania kumpigia kura Mondi bila kutambua kuwa wanaopiga kura ni kundi maalum la watu 500 waliochaguliwa kupitia mchujo maalum.

 

HAKUNA KURA ZA MASHABIKI BET

Ndiyo maana yake kwani wakati mashabiki wa Mondi na Burnaboy wakihangaika kusaka ‘link’ ili wawapigie kura wasanii hao kuwawezesha kushinda Tuzo ya BET katika Kipengele cha Best International Act 2021, Gazeti la IJUMAA limechimba na kubaini mchakato mzima.Ukweli ni kwamba, BET hawana mfumo wa mashabiki kupiga kura (popular votes) ili kumpata mshindi, bali kura zinapigwa na akademi yao (BET Awards Voting Academy) yenye watu 500 ambayo tayari wanakuwa wamewachagua wenyewe.

 

Akademia hii inajumuisha watu mbalimbali wenye uelewa kutoka kwenye muziki, media, bloga, burudani na hata mashabiki ambao hupita katika mchakato maalum kabla ya kutambulika.BET kupitia tovuti yao hutoa taarifa kuwa wanahitaji wanachama wa kupiga kura kisha wanaambatanisha na fomu ya maswali ambayo anayehitaji kuingia katika hiyo akademi atayajibu.

 

Maswali yanalenga kupima uelewa wa mwombaji kuhusu burudani na wale watakaojibu vizuri ndiyo wanaingia katika akademi hii.

 

SIRI YA VITA HII NI NINI?

Yamkini wanaompinga Mondi na kuendesha kampeni ya kutompigia kura wanajua ukweli huo kwamba hawawezi kupiga kura, lakini kuna siri nyingine zaidi iliyo nyuma ya pazia.Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya burudani, siri hiyo kuwa ni kushindanisha makundi ya kimuziki nchini hususan hasimu mkubwa wa Mondi sasa ambaye ni Rajab Abdul ‘Harmonize’ au ‘Harmo’.

 

Uhasama wa Harmo kwa Mondi umeendelezwa na timu yake ambayo inaongozwa na Mwijaku pamoja na msanii mwenzake, Hamis Ramadhani ‘H Baba’ ambao lengo ni kumshusha Mondi kimuziki.

 

Hata hivyo, tayari Mondi amejibu mkakati huo na kuwaeleza kuwa kwa miaka 10 aliyodumu kwenye gemu wapo waliotaka kumuua kimuziki, lakini wameshindwa, hivyo wanaopiga kelele sasa wala hawawezi kufua dafu.

 

HII NI MARA YA TATU

Hii ni mara ya tatu kwa Mondi kuteuliwa kuwania tuzo hizo ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2014 na mara ya pili mwaka 2016 na zote hakufanikiwa kutwaa tuzo hizo.

Stori; Gabriel Mushi, Dar


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad