Morogoro. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim amewaonya madereva wa magari kuacha kuweka maua kwenye magari ili ionekane wanakwenda msibani ili lengo likiwa kukwepa kusimamishwa na askari wa usalama barabarani.
Ameeleza hayo leo Jumanne Juni 22, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajali iliyotokea mkoani humo usiku wa kuamkia leo ikihusisha magari matatu na kusababisha vifo vya watu tisa na majeruhi 24.
Amesema katika ajali hiyo watu watano walifariki hapohapo, wakiwemo madereva wa lori, Selemani Chali na Adamu Minde na abiria aliyefahamika kwa jina moja la Nassor.
Amesema chanzo cha ajali hiyo ni gari aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya likiendeshwa na Minde kutaka kulipita gari jingine aina ya Toyota Cresta lililokuwa likiendeshwa na Emmanuel Sembuche bila kuchukua tahadhari.
Amesema gari hilo liliigonga Cresta na kupoteza mwelekeo na kukutana uso kwa uso la lori hilo mali ya kampuni ya Dangote lililokuwa likiendeshwa na Chali.
“Lile Coaster lilikuwa na mashada ya maua wakiashiria kuwa walikuwa wanapeleka maiti ili askari wasiwakamate. Nawaonya madereva kuacha tabia kama hii, tumejipanga vizuri kuhakikisha udanganyifu kama huo hautokei tena,” amesema.
Wakati huohuo, kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Kessy Ngalawa amesema saa 6 usiku walipokea majeruhi na miili saba na ilipofika asubuhi vifo viwili viliongezeka.
Amesema hadi leo mchana miili mitatu ilitambuliwa na ndugu na kwamba majeruhi watano hali zao si nzuri na wanaendelea kufanyiwa uchunguzi.