MSHAMBULIAJI wa Kaizer Chiefs, Mzambia, Lazarus Kambole, amefunguka kuwa hajui chochote juu ya kutakiwa na Yanga lakini amesisitiza kwa upande wake atakuwa tayari ikiwa utaratibu utafuatwa kwa kuwa bado yeye ni mchezaji wa Kaizer.
Hii si mara ya kwanza kwa mshambuliaji huyo kuhusishwa na Yanga ambapo mwaka 2019 akiwa na Zesco United ya Zambia ilibaki kidogo ajiunge na timu hiyo kabla Kaizer Chiefs kuwazidi Yanga ambapo amejiunga nayo kwa mkataba wa miaka mitatu.
Kwa sasa inaelezwa mshambuliaji huyo amekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo akiwa amecheza mechi 11 za Ligi Kuu ya Afrika Kusini kati ya hizo akiwa ameanza nne huku saba akitokea benchi hali iliyopelekea kutaka kutolewa kwa mkopo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Kambole alisema kuwa: “Kiukweli kwa upande wangu sijaongea na kiongozi wa timu yoyote kutoka huko (Tanzania) au kuzungumza na uongozi wa timu zaidi ya kubaki kuwa kama tetesi kwa sababu sijui na hakuna ambaye amenifuata, inakuwa ngumu kuweza kujua cha kusema.
“Sina shida nao ikiwa watafuata utaratibu ambao unajulikana kwa sababu bado ni mchezaji wa timu nyingine lakini kitu kikubwa ambacho kinatakiwa kufanyika ni kuona wao watafuata utaratibu kwa kiasi gani kutokana na mkataba ambao bado nipo nao hapa kwa sasa,” alisema Kambole.Ibrahim Mussa,Dar es Salaam