Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kuwa inampango mkakati wa kuanzisha utalii wa lugha ya Kiswahili kwenye maeneo yote yenye kumbukumbu kama Butiama kwa lengo la kuwawezesha watalii kujifunza Kiswahili pamoja na kusimuliwa historia na kumbukumbu za waasisi wa Taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 28, 2021, na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Mary Masanja wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Esther Matiko, aliyehoji mpango wa serikali wa kuyaboresha maeneo aliyozaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ili pawe historical site kama ilivyo Afrika Kusini kwa Hayati Nelson Mandela.
"Serikali ina mpango wa kuanzisha utalii wa Kiswahili kwenye maeneo hayo yenye kumbukumbu ili mtalii anapofika katika maeneo hayo ajifunze lugha ya Kiswahili, lakini pia atasimuliwa historia na kumbukumbu ya waasisi wetu walikuwaje na walifanya nini na ukizingatia Mwalimu Nyerere alikuwa ni Muasisi wa kuboresha lugha yetu hii," amejibu Naibu Waziri Mh. Mary Masanja.