Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ameeleza jinsi alivyompigia simu Rais Samia Suluhu Hassan akimtaka wakutane na kwamba yuko tayari kurudi Tanzania endapo maridhiano yatafikiwa.
Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi akiwa jijini Dodoma Septemba 7, 2017 amekuwa akiishi nchini Ubelgiji alikokwenda kupatiwa matibabu.
Julai 2020 alirejea nchini na kugombea urais kupitia Chadema, lakini baada ya uchaguzi huo alioshinda hayati Rais John Magufuli kuisha, alidai kutishiwa maisha na kurudi tena Ubelgiji.
Akizungumza jana jijini Nairobi, Kenya alikokwenda kuzindua kitabu chake kinachohusu demokrasia katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Lissu alisema ameshampigia simu Rais Samia na kuzungumza naye suala hilo.
Alisema ili rais mpya afanikiwe, anapaswa kuruhusu mabadiliko ya Katiba, kutoa uhuru zaidi kwa vyama vya upinzani na kuruhusu maoni tofauti.
“Nilimpigia simu Rais Suluhu siku mbili baada ya kuapishwa na simu yake ilipokelewa na msaidizi wake na nikamwomba amjulishe kuwa nitafurahi kukutana naye na kujadiliana kuhusu mwelekeo wa Tanzania na jinsi tutakavyoiendesha nchi. Bado ninasubiri jibu.
“Hata uongozi wa chama chetu cha Chadema, ukiongozwa na Mwenyekiti ulipeleka ombi kwa Rais ambao ulijibiwa baada ya wiki moja, lakini bado tunasubiri jibu la kikao hicho,” alisema Lissu.
Alisema kusinyaa kwa demokrasia kumekuwa hatari iwe ni kwa muda mfupi au mrefu, akirejea mkakati wa maridhiano wa Kenya (BBI) unaolenga kurekebisha Katiba pamoja na mengine, akisema pamoja na kuwa na sura ya maridhiano, mkakati huo una sura ya kukumbatia madaraka ya urais.
Alisema mchakato wa BBI uliokuwa ukipigiwa chapuo na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga una sura ya udikteta uliojikita katika uongozi wa Tanzania na kuionya nchi hiyo kufuata njia hiyo.
Katika uzinduzi wa kitabu hicho uliohudhuriwa na Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya, Willy Mutunga, viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe na wageni wengine, Lissu alikosoa kile alichokiita kuibuka kwa udikteta na urais wa kifalme katika mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania unaonyanyasa wapinzani.
Katika hotuba yake, Dk Mutunga aliunga mkono kauli za Lissu akisema kumekuwa na tabia ya kuibuka kwa udikteta akisema tabia iyo ni hatari kwa vizazi vijavyo.