Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema Tundu Lissu amesema kwamba yuko tayari kurudi Tanzania ili kufanya kazi na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kwenda mafichoni nchini Ubelgiji baada ya uchaguzi wa mwaka jana.
Kulingana na Gazeti la The Citizen nchini Tanzania, Bwana Lissu alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu chake kipya kuhusu demokrasia Afrika Mashariki, ambapo aalisema kwamba tayari amempigia simu kiongozi huyo mpya wa Tanzania na kuomba kufanya mkutano naye.
Akizungumza mjini Nairobi, Kiongozi huyo ambaye alipoteza uchaguzi wa mwaka jana kwa Hayati John Pombe Magufuli alisema kwamba lengo lake la kupata mkutano wa ana kwa ana na Rais Samia ni kuzungumzia kuhusu kupanua hali ya kidemokrasia ambayo amesema inatia wasiwasi.
Amesema kwamba kwa rais huyo mpya kufanikiwa, mabadiliko ya kikatiba , kutoa uhuru kwa sauti za wapinzani ni muhimu , kitu ambacho uongozi mpya amesema unaweza kujitolea kufanya.
''Nilimpigia simu Rais Suluhu siku mbili baada ya kuapishwa na simu hiyo ilichukuliwa na masaidizi wake , ambaye nilimuomba kumwambia Rais kwamba ningefurahia kuketi naye chini na kuzungumzia jinsi Tanzania itakavyosonga mbele na jinsi tunaweza kubadilisha taifa letu. Lakini bado nasubiri jibu'',Bwana Lissu alinukuliwa na The Citizen Tanzania akisema.
"Hata kiongozi wetu wa chama alimuomba Rais na akajibiwa baada ya wiki moja , lakini bado tunasubiri jibu la kuwa na mkutano," alisema.
Katika kitabu chake alichokizindua ambacho uzinduzi wake ulihudhuriwa na aliyekuwa jaji mkuu wa Kenya Willy Mutunga, viongozi wa Chadema walikosoa kile alichokitaja kuwa kuchipuka kwa uongozi wa kiimla katika mataifa matatu ya Afrika Mashariki , Kenya Uganda na Tanzania ambazo amedai kukandamiza sauti za wapinzani.
Kitabu hicho kwa jina Remaining in the shadows: Parliament and Accountability in East Africa , kinazungumzia kuhusu mifumo ya utawala.
Mambo sita anayotaka ahakikishiwe utekelezaji wake kabla ya kurejea nyumbani
Tundu Lissu amedai hakikisho la usalama wake kutoka kwa serikali,msamaha kwa wafungwa wa kisiasa na kukabidhiwa kwa gari alilopanda katika siku ambayo alinusurika baada ya kupigwa risasi 16 mjini Dodoma.
Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki pia anataka hakikisho la serikali kuwa itamlipa gharama za matibabu aliyotumia, mafao yake kama mbunge wa zamani na kutathminiwa upya kwa kesi dhidi yake.
Bw Lissu alikuwa akizungumza na gazeti la Mwananchi kutoka nchini Ubelgiji ambako alikwenda kwanza kwa ajili ya matibabu mwezi wa Januari 2018 baada ya kushambuliwa na 'watu wasiojulikana' mjini Dodoma.
Kauli za Bw Tundu Lissu zinajiri wakati Rais wa Tanzania Samia Suluhu akiahidi kukutana kwa mazungumzo na viongozi wa upinzani nchini humo, jambo lililopokelewa vyema na viongozi wa upinzani.
Bw Lissu alisema anahofia sana uamuzi wa kumuondolea walinzi wa usalama wake ambao alipewa mwaka 2020 alipogombea kiti cha urais kupitia chama cha Chadema kwani uamuzi huo unatishia maisha yake.