Kifo cha mfanyabiashara mashuhuri nchini Kenya, Chris Kirubi, kilichotangazwa na familia yake Juni 14, 2021, kimeacha simanzi kwa Wakenya na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa marehemu alikuwa anaugua maradhi ya saratani tangu mwaka 2017. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80.
Kirubi alitambulika kama mfanyabiashara shupavu, kiongozi, mshauri na mfano wa kuigwa na wengi.
Alikuwa kati ya watu tajiri zaidi nchini humo akishika nafasi ya tisa kwa kuwa na utajiri wa thamani ya Sh trilioni moja nyuma ya familia ya Uhuru Kenyatta anayeshika nafasi ya nane wakati familia ya Moi ndiyo inayoshika namba moja kwa kuwa na utajiri wa Sh trilioni 5 kwa mujibu wa Forbes.
KAMPUNI ALIZOMILIKI
Na hizi baadhi ya kampuni kubwa za kibiashara ambazo marehemu alimiliki na kuongoza kabla ya kifo chake.
Centum
Kirubi ndiye alikuwa mwenye hisa nyingi katika kampuni ya uwekezaji ya CENTUM.
Kampuni ya Centum inadaiwa kuwa miongoni mwa kampuni zilizo na hisa nyingi zaidi kwenye soko la hisa la Nairobi Securities Exchange.
Mwaka wa 2017, Kampuni hiyo ilizindua jengo kubwa la maduka la Two Rivers kando na barabara ya Limuru baada ya kununua shamba la ekari 100 maeneo hayo ya Kiambuu nchini humo. Centum pia imekita mizizi yake nchini Uganda.
International House Limited
Kirubi alikuwa mkurugenzi mtendaji katika kampuni ya usimamizi wa mali ya International House Limited.
Kampuni hiyo ilianzishwa mwakani 1985 baada ya kununua jumba la International House kutoka kwa kampuni ya Canada.
Bayer East Africa LTD
Kirubi alikuwa naibu mwenyekiti katika kampuni ya Bayer East Africa Ltd.
Kampuni ya Bayer East Africa LTD inahusiana na utafiti na ubunifu wa Kisayansi kwenye nyanja za ukulima na afya. Ina maskani pia nchini Ujerumani.
Bayer East Africa ambayo ina makao yake makuu ni jijini Nairobi imepanuka hadi nchini Ethiopia, Tanzania, Uganda na Rwanda.
HACO Tiger Brands (EA) LTD
Kirubi ndiye mmiliki wa kampuni ya Haco Tiger Brands ambayo inahusiana na nguo, viatu, kalamu, vipodozi, vifaa vya stima, bidhaa za plastiki, kemikali na biashara zingine.
Bidhaa za kampuni hiyo ambayo ilianzishwa mwaka wa 1974 zinauzwa hadi nje ya mipaka ya Kenya.
DHL Worldwide Express Ltd
Kirubi alimiliki kampuni ya usafirisha ya DHL Worldwide Ltd.
Kampuni hiyo inahusika na kusafirisha vifurushi katika zaidi ya mataifa 220 duniani
Capital Media Group
Kirubi alinunua kampuni ya Capital Media Group ambayo inamiliki Kituo cha redio cha Capital FM mwaka wa 2014.
Aliwashangaza wengi baada ya kujitangaza kuwa mmoja wa wacheza santuri katika stesheni hiyo na kujipa jina la usanii ‘DJ CK’
Bilionea huyo aliwahi kukiri kuwa alinunua stesheni ya Capital kwa sababu kampuni yake ilikuwa inatumia pesa nyingi kufanya matangazo kituoni hapo.
Katika mahojiano kwenye kipindi cha Churchill Show mwezi Septemba mwaka uliopita, Kirubi alisema kuwa mapenzi yake kwa muziki wa ujana yalimfanya kununua stesheni hiyo.
Nairobi Bottlers
Kampuni ya Nairobi Bottlers ambayo ilimilikiwa na Kirubi inahusiana na utengenezaji na usambazaji wa vinywaji ikiwemo bidhaa za kampuni ya Cocacola.
Maji ya Keringet, juisi ya minute maid na kahawa ya Fuze ni baadhi ya bidhaa za kampuni hiyo.
Smart Applications International Ltd
Kirubi pia alimiliki kampuni ya kiteknolojia ya Smart Applications.