MSHAMBULIAJI wa kikosi cha Mbeya City, Kibu Denis amekiri kuwa kuna uwezekano mkubwa wa yeye kumalizana na Yanga, kutokana na hatua nzuri ambayo mazungumzo yao yamefikia mpaka sasa, huku pia akiweka wazi kuwa wazazi wake wamefurahi kusikia uwezekano wa kukamilika kwa dili hilo.
Uwezo mkubwa wa nyota huyo umezifanya klabu vigogo za Simba na Yanga kuingia vitani kusaka saini yake, ambapo mpaka sasa tayari uongozi wa Mbeya City kupitia kwa Katibu Mkuu wake Emmanuel Kimbe, umekiri kuwa kwenye hatua za mwisho za mazungumzo na uongozi wa Yanga, huku pia Simba wakitajwa kupeleka ofa ya kumsajili kiungo huyo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Kibu alisema: “Ni kweli niko kwenye mazungumzo mazuri na Yanga kuhusu mpango wa kujiunga nao na mpaka sasa wanasubiri majibu yangu, lakini nisingependa kuzungumza mambo mengi kuhusiana na usajili kwa sasa kwa kuwa mimi bado ni mchezaji wa Mbeya City.
“Lakini kwa kuwa mimi ni mchezaji, chochote kinaweza kutokea kama Mungu akipenda basi naweza kuwa sehemu ya kikosi chao msimu ujao, kwa kuwa hiyo itakuwa ni hatua nyingine kubwa kwangu, na hata wazazi wangu wamefurahi kusikia nahitajika Yanga.”
Joel Thomas,Dar es Salaam