Waziri wa Afya wa Uingereza Matt Hancock amekiri kuvunja masharti ya kutokaribiana baada ya kupigwa picha akimbusu mmoja wa wasaidizi na picha hiyo kuchapishwa kwenye gazeti moja.
Alisema kwamba "amewaangusha watu" baada ya kuonekana kwenye picha akiwa na Gina Coladangelo - aliyemteua - na kuomba "msamaha".
Chama cha Labour kimemuomba Waziri Mkuu kumchukulia hatua Bwana Hancock, kikitaja nafasi aliyopewa kuwa amepewa mtu"asiyefaa".
Lakini Bwana Boris Johnson amesema kwamba ameukubali msamaha wa Bwana Hancock na "kuchukulia kuwa suala hilo limeisha".
Waziri Mkuu aliulizwa kama "ana imani" na Bwana Hancock, msemaji wa Waziri Mkuu alijibu: "Ndio."
Gazeti la The Sun limeripoti kuwa picha za Bwana Hancock na Bi Coladangelo, ambao wote kila mmoja ana familia yake na wana watoto zilipigwa wakiwa ndani ya ofisi za Wizara ya Afya mapema mwezi Mei.
Kutokaribia katika maeneo ya kazi sio sheria ila ni sharti lililopendekezwa na serikali.
Watu wanashauriwa kuhakikisha wanatimiza kanuni ya kutokaribiana umbali na mita 2 inapowezekana au mita 1 kama hatua ya kupunguza hatari iliyopo.
Mei 6, England ilipokuwa bado katika hatua ya pili ya kukabiliana na kanuni zilizowekwa kupambana na virusi vya corona, kutangamana katika eneo la ndani kwa madhumuni ya kikazi kuliruhusiwa lakini iwapo tu "kutakuwa na haja ya kufanya hivyo".
Mwenyekiti wa chama cha Labour Annaliese Dodds alisema: "Ikiwa Matt Hancock amekuwa na uhusiano wa kisiri na mshauri wake ofisini - ambaye yeye mwenyewe alimteuwa kutekeleza majukumu ambayo yanasimamiwa na mlipa kodi kimshahara - ni utumiaji mbaya wa wazi wa madaraka na wenye kuleta mgongano wa kimaslahi.
"Makosa dhidi ya Matt Hancock ni pamoja na kutumia vibaya kodi ya mwananchi, kuweka eneo la utoaji huduma katika hatari na sasa kushutumiwa kwa kuvunja mwenyewe kanuni zilizowekwa kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona.
"Kwa nafasi yake hawezi kutetewa. Boris Johnson anastahili kumfuta kazi."
Msemaji wa serikali amesema kuteuliwa kwa Coladangelo "kulifanyika kwa njia ya kawaida "na kulifuata mchakato stahiki".
Katika taarifa Bwana Hancock, 42, baba wa watoto watatu, alisema: "nakubali kwamba nimekiuka sharti la kuutokaribiana katika hali hii. Nimewaangusha watu na naomba msamaha.
"Nitaendelea kuangalia namna ya kuhakikisha nchi yetu inakabiliana na janga hili, na nitashukuru ikiwa nitapewa faragha na familia yangu kuhusiana na suala hili."
Bwana Hancock alifuta ziara yake ya kutembelea kituo kinachotoa chanjo ya corona cha Newmarket Racecourse, Ijumaa asubuhi, saa kadhaa baada ya gazeti la the Sun kuchapisha taarifa hiyo.
Bi. Coladangelo, ambaye amekuwa akifahamiana na waziri huyo wa afya tangu walipokuwa wakifanya kazi pamoja katika kituo kimoja cha shule chuo kikuu cha Oxford, aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa wiizara ya afya mnamo mwezi Septemba lakini sio miongoni mwa watendaji wakuu.
Jukumu analotekeleza mshahara wake ni pauni 15,000 kwa siku 15 hadi 20 za kufanyakazi kwa mwaka.
Chama cha Liberal Democrats kilitoa wito kwa Bwana Hancock kujiuzulu na kumshutumu kwa "unafiki" kuhusiana na suala la kutokaribiana.
Msemaji wa wizara ya afya Munira Wilson alisema: "alikuwa akielezea familia kwamba zisikumbatie wapendwa wao huku akiwa anafanya kile anachokipenda akiwa kazini."
Waziri wa usafirishaji Grant Shapps ameelezea BBC Radio 4 katika kipindi cha Today programme kwamba: "Nafkiri kwa kipindi kirefu kumekuwa na utofauti kati ya kile ambacho watu wanafanya wakiwa kazini ... na kile wanachofanya katika maisha yao ya kibinafsi."
Bwana Hancock amekuwa katika ndoa kwa miaka 15 na Martha, ambaye ni mtaalamu wa tiba. Bi. Coladangelo, 43, naye ameolewa na Oliver Bonas mwanzilishi wa kampuni ya Oliver Tress.
Ijumaa, Waziri wa Kwanza wa Wales wa chama cha Labour Wales Mark Drakeford alisema kuwa Bwana Hancock amekuwa wa kwanza "kumshutumu" Profesa Ferguson, na kuongeza kuwa: "Hapa Wales, bila shaka yoyote natarajia timu yote ya mawaziri kufuata kanuni ambazo tunatarajiwa watu wengi wazifuate.
"Hatuwezi kutengeneza sheria kwa ajili ya wengine na sisi wenyewe tuwe hatuko tayari kuzifuata.