Baada ya maduka na majengo kuchomwa moto siku ya Jumatatu, wakati Zuma akisikiliza kesi yake katika mahakama ya juu serikali ya Afrika kusini imepeleka jeshi kukabiliana na ghasia zinazoendelea baada ya Zuma kufungwa.
Watu wapatao sita wameuawa na 200 kukamatwa tangu ghasia hizo zilipoanza wiki iliyopita.
Zuma amehukumiwa kwa kosa la kuidharau mahakama baada ya kushindwa kuhudhuria kesi yake ya madai ya rushwa wakati wa utawala wake.
Zuma mwenye umri wa miaka 79, ambaye alikanusha kuhusika katika madai ya rushwa, lakini alienda mwenyewe polisi wiki iliyopita ili kuanza kifungo chake cha miezi 15 wakati akiwa anatarajia kifungo chake kupunguzwa katika mahakama ya katiba, hata hivyo wataalamu wa sheria wanasema nafasi ya kushinda ni ndogo sana.
Jumatatu, picha za video zilionesha maduka makubwa yakichomwa moto katika mji wa Pietermaritzburg, katika eneo alikotokea Zuma, KwaZulu-Natal, na watu wakifanya maandamano na ghasia zilienea mpaka Johannesburg, katika jimbo la Gauteng.
Jumapili, waandamanaji walionekana wakiandamana katika maeneo ya biashara ya mjini Johannesburg.
Jeshi la Afrika Kusini limesema limeagizwa kwenda kusaidia kupunguza ghasia ambazo zimekuwa zikiendelea kwa siku kadhaa huku Rais Cyril Ramaphosa akisisitiza utulivu na kusema hakuna maelezo juu ya vurugu hizo.