Aliyeng’ara UMISSETA ala shavu Marekani





Mwanafunzi Benedict Mathias kutoka shule ya sekondari ya Filbert Bayi ya Pwani ambaye aling’ara katika mashindano ya mbio fupi za mita 100, 200, na 400 kwenye michezo ya UMISSETA iliyomalizika hivi karibuni katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Mtwara ni miongoni mwa wanariadha wanne kutoka Tanzania wataokwenda nchini Marekani kwa ajili ya masomo.

 Ben ambaye hukimbia mithili ya ‘Usain Bolt, mwanariadha wa kimataifa wa Jamaica atakwenda nchini Marekani mwakani pindi atakapomaliza masomo yake ya kidato cha nne huku wanafunzi wenzake watatu wakitangulia mwaka huu.

Akizungumza katika siku ya mwisho ya mashindano ya riadha katika michezo ya UMISSETA mwaka huu yaliyomalizika hivi karibuni mjini Mtwara mmiliki wa shule hiyo ya vipaji vya michezo, Filbert Bayi amesema mwanafunzi wa kike wa shule hiyo anatarajia kwenda Marekani mwezi wa nane mwaka huu.


“Binti yetu mmoja tayari amepata ufadhili wa masomo na anajiandaa kwenda Marekani ‘Northern Corolado University’ kwa ajili ya masomo na kuendeleza kipaji chake cha kukimbia,” alisema.

Alisema Tanzania inawategemea wachezaji hawa kufanya vizuri katika mashindano yajayo ya Afrika, Jumuiya ya Madola, na Olimpiki 2024.

Alisema kuwa wanawatafutia wanafunzi hao nafasi za kwenda Marekani kwasababu Marekani wanahitaji wanafunzi wenye vipaji lakini pia nchi hiyo imetengeneza mazingira ya kukuza vipaji vya wanariadha kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Wamarekani wanataka wachezaji kutoka Afrika kama zamani ilivyokuwa, sisi tumesoma Marekani, Nyambui amesoma Marekani, kina Shahanga na wengine wengi wote tumesoma Marekani,” alisisitiza Bayi na kuongeza:

“Wenzetu kule wana ‘high performing centres’, na wana ‘high performing coaches’ na watasaidia kwani nchi kama Jamaica, Bahamas wachezaji wao wamesoma Marekani, na ndiyo maana wanafanya vizuri.”

Bahi alisema siyo kwamba Tanzania haina walimu wa  riadha, bali kiwango chao bado kipo chini kulinganisha na mataifa yaliyopiga hatua katika mchezo wa riadha, hivyo akawataka walimu wa riadha nchin wasisite kuomba mafunzo ya riadha yanapojitokeza na kamati ya Olimpiki Tanzania itaweza kujenga hoja ili wapate fursa hizo.

Katika mashindano ya UMISSETA yaliyomalizika hivi karibuni wanariadha kutoka mikoa mbalimbali nchini waling'ara katika michezo hiyo, na kuzivutia baadhi ya taasisi nchini kuahidi kuwachukua wanafunzi hao kujiunga na taasisi hizo pindi watakapohitimu masomo yao ya kidato cha nne.

Caption

Mwanariadha Benedict Mathias wa pili kulia akichuana vikali na wanariadha Kassim Khamis wa Unguja (kulia) na wanariadha wengine walioshiriki fainali za mbio za mita 100 UMISSETA ambapo Benedict alishinda mbio hizo.

Wanariadha kutoka mikoa mbalimbali wakichuana katika fainali za mbio za mita 800 zilizomalizika hivi karibuni mkoani Mtwara.

Mwanariadha Benedict Mathias akipozi kabla ya kukimbia mbio za mita 400 ambapo alishika nafasi ya kwanza katika mashindano yaliyomalizika hivi karibuni mkoani Mtwara

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad