JAMII imeonywa kuhusu kuendeleza imani na dhana potofu zinazopuuza kanuni za kujikinga na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU).
Angalizo hilo limekuja baada ya binti mwenye umri wa miaka 24 aliyekuwa anaishi na VVU, kumwambukiza bibi yake mwenye umri miaka 78 mkoani Mtwara.
Mtafiti Mkuu, Dk. Pedro Pallangyo, alibainisha mkasa huo jana mkoani Dar es Salaam, akiwasilisha matokeo ya utafiti kuhusu Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI Toka kwa Binti wa Miaka 24 Kwenda kwa Bibi yake Mwenye Umri wa Miaka 78.
Dk. Pedro ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya ndani na bingwa wa afya ya jamii na mtafiti, alisema ni muhimu jamii kuendelea kutambua kwamba maambukizi ya VVU yanaendelea katika jamii zetu, hivyo hatua zichukuliwe na kufuata maagizo ya kitaalamu.
Alisema kanuni za kujikinga na VVU zinafahamika kwenye jamii kwamba ni kuepukwa kuchangia vitu vyenye ncha kali, ikiwamo sindano, wembe na kuepukwa ngono zembe.
Alisema utafiti wao ulibaini bibi huyo alitumia mbinu zisizo salama kumuuguza mjukuu wake huyo pasipo kuvaa vifaa maalum kujikinga.
"Pamoja na kuendelea kujikinga kwa njia kuu zinazojulikana, yaani kuepuka ngono zembe, ni muhimu kutambua kuwa kuna mila na tamaduni mbalimbali zinazoweza kuchochea kusambaa kwa maambukizi," alisema.
Bingwa huyo alisema kuwa tangu mwaka 1981, VVU vimeathiri watu milioni 77 duniani na kwamba mara nyingi maambukizi hupitia njia tofauti ikiwamo kujamiiana, kuchangia vitu vya ncha kali kupitia damu na mtoto anapozaliwa.
Dk. Pedro alibainisha kuwa bibi wa miaka 78, mkazi wa Mtwara, alifikishwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), akitibiwa na ana historia ya miaka 35 akiugua 'hypertension' na kwamba mara ya mwisho alihudhuria JKCI miezi 11 iliyopita na alikuwa hana maambukizi ya VVU.
"Alifika (bibi) kwetu akiwa na tatizo la uzito kupungua, homa za mara kwa mara, na kikohozi. Baada ya vipimo ilibainika ameathirika, na kuchunguza ikabainika alikuwa anaishi na mjukuu wake wa miaka 24.
"Binti alipewa talaka, na historia yake alikuwa na homa mara kadhaa, uzito kupunguza na maradhi ya ngozi. Bibi yake alimhudumia kwa mikono yake bila kujikinga.
"Na walipopimwa wakabainika na kukutwa na maambukizi, wote wakawa wanatumia dawa. Binti alifariki dunia wiki 12 zilizopita.
"Imani zilizopo katika jamii, watu wakiamini wanasambaza upendo na ukaribu hasa Waafrika, huchangia kusambaa kwa maambukizi hususan nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Elimu bado inahitajika," alisema.
Dk. Pedro alishirikiana na mabingwa wengine kwenye utafiti huo, akiwamo Prof. Mohamed Janabi, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI.