Rais wa Marekani Joe Biden amesema kila mwananchi atakaekubali kupigwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 atalipwa dola 100. Marekani ni nchi yenye chanjo za kutosha, na idadi kubwa ya watu wanaopinga kuchanjwa.
Rais wa Marekani Joe Biden amewashauri viongozi wa majimbo na miji yote nchini humo kuwalipa wakazi wao dola 100 ili wapigwe chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.
Aidha ameweka sheria mpya zinazohitaji wafanyakazi wote wa serikali kuonyesha uthibitisho wa kupigwa chanjo au kulazimika kupimwa ugonjwa huo mara kwa mara, kuvaa barakoa pamoja na kuwekewa vikwazo vya kusafiri.
Hatua hizo za hivi karibuni ni miongoni mwa juhudi za Biden kujaribu kuwahamasisha Wamarekani wenye kupiga chanjo, huku aina mpya ya virusi vya corona iitwayo Delta ikiwa inaenea kote nchini humo, hasa miongoni mwa watu ambao bado hawakuchanjwa.
Marekani inashika mkia miongoni mwa nchi zilizoendelea kwa viwango vya watu waliochanjwa, licha ya kuwa na chanjo za kutosha zinazotolewa bure. Juhudi za Ikulu ya Marekaniza kuhamasisha wananchi kuchanjwa zimegonga ukuta, hasa kutokana na vuguvugu kubwa linalopinga chanjo hiyo, habari za uwongo zinazosambazwa kuhusu chanjo pamoja na migawanyiko ya kisiasa.
Uamuzi wa Biden kuhitaji mamilioni ya wafanyikazi wa serikali na makandarasi kuonyesha uthibitisho wa kupigwa chanjo unaonyesha kuwa Ikulu imeamua kuchukua msimamo mkali zaidi huku virusi hivyo vya aina ya Delta vikiwa vinazidi kuenea.
Biden amewaambia waandishi wa habari wa Ikulu, kwamba watu wengi sana wanafariki dunia au wanapoteza watu wanaowapenda.
Kulingana na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), takribani watu milioni 163.8 nchini Marekani ndiyo waliochanjwa dozi kamili ya chanjo kati ya idadi ya watu milioni 330.
Serikali ndiye mwajiri mkubwa zaidi nchini Marekani, na hatua ya Biden inaweza kuwa mfano wa kuigwa na makampuni binafsi ya kibiashara na taasisi nyingine wakiwa wanajitayarisha kurudisha wafanyakazi maofisini.
Wafanyakazi wa serikali ambao watashindwa kuonyesha uthibitisho wa kuchanjwa watalazimika kupimwa ugonjwa wa COVID-19 kila wiki au mara mbili kwa wiki pamoja na kuwekewa vikwazo vya kusafiri.
Wizara ya Fedha imesema serikali za majimbo zitatumia dola bilioni 350 zilizotengwa kwa ajili ya kupambana na corona kuwalipa wananchi dola 100 kila atakaekubali kupigwa chanjo ya kuwakinga na ugonjwa huo wa COVID-19.
Biden amesema anafahamu kuwa wale ambao tayari wameshachanjwa hawatofurahichwa na umauzi huo, lakini amelazimika kuchukua hatua hiyo ili kuwalinda Wamarekani wote.