CCM yawaonya madiwani wanaowaingilia wakurugenzi





Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro kimewataka madiwani kutambua mipaka yao ili wasiingilie majukumu ya wengine.


Rai hiyo imetolewa leo Jumamosi Julai 17 na Mwenyekiti wa CCM mkoa, Patrick Boisafi alipofungua semina ya madiwani na wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro.



Boisafi amesema kumekuwapo na sintofahamu katika utendajikazi kati ya madiwani na watendaji wa kata, vijiji na wakurugenzi katika baadhi ya halmashauri jambo ambalo lisipodhibitiwa linaweza kukigharimu chama katika uchaguzi mkuu ujao.



"Ni vizuri tukaheshimiana ndani ya utekelezaji wa kazi tunazozifanya, tusipofanya hivyo tunatengeneza mazingira ya watu kutumia mapungufu yetu kutusema kwenye majukwaa, chama hakijabadilisha mfumo wa utaratibu na muundo wa uongozi," amesema Boisafi.



"kwa hali iliyopo amesema watendaji wanaona kama wanaitumikia Serikali tofauti na ile wanayoitumikia watendaji wa kata na baadhi ya wenyeviti wa vijiji. Vilevile, amesema zipo tofauti kati ya baadhi ya wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri utafikiri mkurugenzi anatoka Serikali hii na madiwani Serikali nyingine na akawakumbusha kwamba Mkoa wa Kilimanjaro umeundwa na Serikali inayotokana na Chama cha Mapinduzi.



Aidha amewataka madiwani kumshauri mkurugenzi na si kuingilia majukumu yake ili kutimiza malengo ya kuwatumikia wananchi.



"Diwani fanya kazi yako ya udiwani na siyo ya mkurugenzi, ninyi simameni kama washauri ili kuhakikisha tunafanikiwa katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi," amesema mwenyekiti huyo.



Boisafi ametumia nafasi hiyo pia kuwataka wakuu wa wilaya kuhakikisha viongozi wa vijiji, mitaa, kata na madiwani wanashirikiana ili kuweka mazingira ya chama kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.



Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Seleman Mfinanga amewataka wabunge na madiwani kushirikiana kuhakikisha utekelezaji wa ilani unatekelezwa kikamilifu.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad