Chanzo cha kifo cha Mchungaji Ambilikile Mwasapile (86) maarufu kwa jina la Babu wa Loliondo, kimeelezwa kuwa aliugua nimonia kali ambayo ilimsababisha kupata tatizo la upumuaji na homa.
Kifo cha Babu wa Loliondo kimetokea jana Julai 30, 2021, katika kituo cha Afya cha Digodigo baada ya kuugua ghafla.
Kwa mujibu wa Eatv.tv. Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala, amesema kuwa taarifa za awali za madaktari zinaeleza chanzo cha kifo ni nimonia ambapo kwa takribani siku tano alikuwa anaumwa na kupata sindano za masaa.
“Jana asubuhi aliamka vizuri akiendelea na matibabu lakini majira ya saa 8:00 mchana alianza kujisikia vibaya ndipo ilitafutwa gari kutaka kumpeleka hospitali ya Wasso ambayo alikuwa akiitaka, lakini alianza kujisikia vibaya na ndipo wakamkimbiza kwenye kituo cha afya cha Digodigo,” amesema Mangwala.
Jina la Babu wa Loliondo lilianza kuwa maarufu masikioni mwa watu wengi duniani tangu mwaka 2011, alipoanza kutoa kikombe cha dawa ambayo yeye alidai kuoteshwa na Mungu kwa ajili ya kutibu maradhi mbalimbali na watu wengi walimiminika kwake kunywa kikombe hicho.