MKURUGENZI wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, ameonya kwamba ulimwengu uko katika “kipindi hatari” cha janga la COVID-19.
Hii ni kutokana na virusi sugu aina ya Delta vinavyozidi kubadilika na kufanya mambo kuwa mabaya zaidi.
“Mataifa maskini yenye kiwango cha chini cha usambazaji wa chanjo, ambayo yanashuhudia matukio ya kushtusha ya hospitali kufurika wagonjwa, yamekuwa yakiendesha mambo kwa njia za kawaida.
Huku hali ikihatarishwa zaidi na aina ya virusi vinavyosambazwa upesi kama vile Delta ambavyo vinazidi kusambaa pakubwa katika mataifa mengi, tuko katika kipindi hatari cha janga hili.’Bado hakuna taifa lililo salama.
Virusi aina ya Delta ni hatari na vinaendelea kubadilika, jambo linalohitaji kutathmini na kubadilisha kwa makini mikakati ya afya ya umma,” alisema Ghebreyesus, kupitia taarifa Ijumaa.
Akifafanua kuwa virusi aina ya Delta vimegunduliwa katika mataifa 98 na kwamba vinasambaa kwa kasi katika nchi zenye kiwango cha chini na cha juu cha usambazaji chanjo, alisema kuna njia mbili muhimu kwa mataifa kuepuka mikurupuko mipya.
“Afya ya umma na mikakati ya kijamii kama vile mikakati thabiti ya kuchunguza, kupima na kugundua visa mapema, kutenga na kutoa huduma muhimu,” alisema.
Alifafanua kuwa kuvaa maski, kudumisha umbali wa kutangamana kijamii, kuepuka sehemu zenye misongamano ya watu na kuwa na sehemu za kuruhusu hewa ndio msingi wa hatua zote za kudhibiti gonjwa hilo.
Ghebreyesus alisisitiza kwamba ulimwengu ni sharti ugawane vifaa vya kujikinga, hewa ya oksijeni, vipimo, tiba na chanjo.
Aliwahimiza viongozi kote duniani kushirikiana ili kuhakikisha kwamba kufikia wakati huu mwaka ujao, asilimia 70 ya watu katika kila nchi watakuwa wamepewa chanjo.
‘Hii ndiyo njia bora zaidi ya kupunguza janga, kuokoa maisha, kuendesha mikakati ya kufufua uchumi kote duniani na wakati huohuo kuzuia kuzuka kwa aina nyingine hatari zaidi za virusi. Kufikia mwisho wa Septemba hii, tunatoa wito kwa viongozi kutoa chanjo kwa asilimia 10 ya watu katika mataifa yote,” alisema.
Huku viwanda vipya vikiwemo vinavyounda chanjo za zmRNA, vikizidi kuanzishwa, bosi huyo wa WHO alisema mikakati hiyo inaweza ikaharakishwa kupitia usambazaji wazi wa teknolojia na maarifa baina ya kampuni.
“Ninahimiza hasa kampuni hizo – BioNTech, Pfizer na Moderna – kusambaza ujuzi wao ili tuharakishe uundaji wa chanjo mpya,” alisema.