Dadeki..Bocco, Morrison waachiwa msala kuwamaliza Yanga



TAKWIMU bora za washambuliaji Bernard Morrison na John Bocco zinaonyesha wanakuwa tishio zaidi ugenini wakati Simba ikijiandaa kuivaa Yanga katika fainali ya Kombe la Shirikisho mjini Kigoma, kesho Jumapili.
boco morison pic
TAKWIMU bora za washambuliaji Bernard Morrison na John Bocco zinaonyesha wanakuwa tishio zaidi ugenini wakati Simba ikijiandaa kuivaa Yanga katika fainali ya Kombe la Shirikisho mjini Kigoma, kesho Jumapili.

Wakati Simba ikifunga mabao 78 kwenye Ligi Kuu, wawili hao ndio wamekuwa moto wa kuotea mbali timu hiyo inapokuwa ugenini hasa nje ya Dar es Salaam kutokana na makali yao ya kufumania nyavu ingawa wapo wenzao ambao hufanya hivyo pia.

Data za Ligi Kuu msimu uliomalizika, zinaonyesha kwamba Bocco aliyemaliza akiwa kinara wa ufungaji katika Ligi na mabao yake 16, amefumania nyavu mara nyingi ugenini kuliko katika uwanja wa nyumbani.

Katika viwanja vya ugenini, Bocco amepachika mabao tisa huku akifunga mabao saba katika uwanja wa nyumbani.


Bocco anafuatiwa na Chris Mugalu, Medie Kagere na Bernard Morrison ambao kila mmoja amefumania nyavu mara nne katika viwanja vya ugenini.

Hata hivyo tofauti na Kagere na Mugalu, Morrison yeye mabao yake manne ni ya kipekee kwani ameyafunga dhidi ya timu nne tofauti akipachika bao moja katika kila mchezo.

Miquissone hatabiriki

Wakati Bernard Morrison akiweka rekodi ya kufunga mabao manne dhidi ya timu nne tofauti katika viwanja vinne tofauti vya ugenini, mshambuliaji Luis Miquissone yeye anaonekana sio mchezaji anayetabirika kwani amekuwa na uwezo wa kufunga mbele ya mabeki wa timu nyingi tofauti na katika viwanja tofauti.


Nyota huyo raia wa Msumbiji yeye ameweka rekodi ya kufunga mabao tisa katika mechi tisa tofauti ambapo katika kila mchezo amepachika bao mojamoja.

Mechi hizo tisa ambazo Miquissone alipachika bao moja katika kila mchezo ni mbili dhidi ya JKT Tanzania, Kagera Sugar, Prisons, Mbeya City, Polisi Tanzania, Dodoma Jiji na Mtibwa Sugar.

Kagere, Mugalu tishio Dar

Chris Mugalu na Medie Kagere ndio vinara wa kupachika idadi kubwa ya mabao kwa mechi ambazo Simba imecheza katika viwanja vya hapa Dar es Salaam ingawa wamekuwa sio tishio kubwa nje mikoani.

Kati ya mabao 15 ambayo Mugalu amefunga kwenye Ligi Kuu, mabao 11 kayafungia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa huku mabao manne tu akifunga huko mikoani.


Kwa upande wa Kagere yeye, mabao 10 amepachika katika viwanja vya Dar es Salaam ambavyo ni Benjamin Mkapa na Chamazi na matatu tu akifunga viwanja vya mikoani.

Mastaa 13 wampa jeuri Gomes

Katika mabao 78 ambayo Simba imefunga kwenye Ligi Kuu msimu huu, ni wachezaji 14 tu ambao wamepachika mabao yote hayo na kati ya hao, 13 anao kikosini katika maandalizi ya mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga huku mmoja tu ambaye ni Ibrahim Ajibu akiwa hayupo kwenye mipango yake baada ya mkataba wake kumalizika.

Nyota hao 13 wa Simba ambao wameifungia mabao timu hiyo kwenye Ligi Kuu msimu uliomalizika ni Bocco aliyefunga mabao 16, Mugalu (15), Kagere (13), Miquissone (9), Clatous Chama (8), Morrison (4), na Mohamed Hussein, Hassan Dilunga, Said Ndemla, Mzamiru Yassin na Rally Bwalya ambao kila mmoja amepachika mabao mawili huku Joash Onyango na Pascal Wawa ambao kila mmoja amepachika bao moja kama ilivyo kwa Ajibu.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema amefurahishwa na ufanisi wa timu yake hasa katika kufumania nyavu na anaamini utakuwa chachu kwao kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho.


“Tuna kikosi bora chenye wachezaji ambao wanajitoa kwa ajili ya timu na kila mmoja anafanya vyema kila anapopatiwa nafasi. Nafurahi kuona tumetwaa ubingwa wa Ligi Kuu tukiwa timu iliyofunga idadi kubwa ya mabao na kuruhusu kufungwa mabao machache.

“Kwa sasa akili yetu tumeielekeza katika mechi yetu ya fainali dhidi ya Yanga. Malengo yetu ni kutwaa ubingwa na naamini hilo linawezekana,” alisema Gomes.

Kocha wa Lipuli ya Iringa, Meja Mstaafu Abdul Mingange alisema Simba ina ubora wa kitimu na wa mchezaji mmojammoja ndio maana imekuwa ikifanya vyema mara nyingi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad