Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesema kutokana na matatizo yanayowakumba watoto wakike anatamani jando na unyango vingerudi huku akipiga marufuku ukeketaji.
Mhe. Gekul amesema hayo katika maombi ya kimila yalioandaliwana Wazee wa kimila wilayani Babati wakiungana na viongozi mbalimbali wa serikali na wa vyama kwa ajili ya kuokoa vijana waliokosa maadili hadi kusababisha kuvunjika kwa ndoa zao.
“Nilitamani jando na unyago irudi lakini ukeketaji tusiuweke humo ndani, natamani wazee wetu binti anapoolewa wazee na mama zetu tuende tukamfunde mtoto mambo gani ya kuvumilia, mambo gani yakifika mwisho basi tufanye nini, leo mabinti wengi wanahangaika wakiwa hawana masaada popote, taifa letu kuna wanawake wengi wanatamani ndoa zingekuwa za mikataba kama wenzetu wa nje kwa maumivu wanayopitia,” amesema Mhe. Gekul.
Wazee hao wa kimila wameeleza kuwa maombi ni kutokana na ndoa nyingi za vijana kutokudumu ilihali vijana wengine kupendelea kulelewa na wanawake kutokana na kutokutaka kufanya kazi badala yake wanataka kuzurura mitaani huku wakifanya ardhi ya Babati kuoneka kama vile imelaaniwa.